Monday, 1 July 2013

KUELEKEA RAMADHANI NA MIMI MUISLAM

Na  MIMI NI MUISLAMU

WASIA WA RAMADHANI

Mwezi wa Ramadhani umewasili inshaallah panapo majaaliwa tufike na kufunga kwa afya na siha kamili.Mema tuyakimbilie kwa wingi na maovu tuyawache.

Lakini hatuna budi kukumbushana kuwa SHEITANI yumo katika harakati zake za mwisho mwisho kabla ya kutiwa minyororo na kufungwa.

Anafanya jitihada kwa kadiri awezavyo ili atuwachie WASIA wa kutekelezwa wakati yeye akiwa kifungoni.Wasia wake kwa binadamu kuyaendeleza yote aliyowaamrisha kuyafanya na kuyapuuza aliyoteremsha Allah (s.w.t),Mungu atunusuru na hayo.

Hivi sasa sheitani anahimiza wafuasi wake watayarishe michezo,ngoma,filamu na mambo mengine ambayo yatamtoa binadamu katika ibada ya kumuabudu Allah na kumuabudu yeye sheitani.

Watu wameanza kutayarisha filamu na programu za kila aina(maasi) kwa aijili ya mwezi wa Ramadhani.Viwanja vya michezo vinatayarishwa na mashindano kuandaliwa kwa ajili ya mwezi huo.

Wanao cheza karata,bao na michezo mengine wote hao Sheitani anawapa fikra zake zote ili watimize maamrisho yake sawa sawa.Imefika hadi watu wako tayari kumchangia sheitani michango ya pesa ili awapoteze vizuri.

Wako tayari kugharimika kwa gharama yoyote ile wala hawaulizi bali hutoa tu.Lakini utapowagusa kwa michango ya kheri na barka wanaruka kwa kuipinga na kuitolea kila sababu za kuitia ila na kasoro.

Mwenyezi Mungu ametuahidi malipo marudufu kwa matendo yote mema kuzidishiwa ujira katika mwezi huu mtukufu.

Na sheitani anafungwa ili kuzuiwa kuwatia wasi wasi binadamu katika ibada zao na kuwapoteza.Kwahio hana la kufanya ila kuwashawishi watu na maasi yote kabla ya Ramadhani wajitayarishe kisawasawa hata yeye akiwa kifungoni mambo yake yawe yanakwenda.Hushangai ukiwaona watu katika mwezi wa ramadhani wanakesha usiku kucha na michezo,filamu na mambo mengine ya upuuzi na kuwaacha ibada ya Mola wao ?

Hawa ni mateka wa sheitani,amewateka nyoyo zao hawasikii hawaoni.Analo sema sheitani ndilo,analosema Muumba wao wanalikanya.

Hasara ilioje hii,kumkataa na kumpinga wazi wazi Muumba wako alokupa roho,uhai na neema zake zote,ukamfuata yule ambae ana uadui wa dhahiri na wewe.

Binadamu ni mwenye kukhasirika kubaya kabisa anapowacha maarisho ya Mola wake na kufuata maarisho ya adui yake ambae anamtakia shari ya kuangamia kama alivyo kwisha angamia yeye.

Tujitahidi kufanya mema mengi zaidi kwa kadiri ya uwezo wetu katika mwezi kama vile:

1.Kusali sala za usiku.

2.Kutoa sadaka kwa muombaji na asie omba.Kuna baadhi ya watu wanawatia ila waombaji kwa kusema hawastahiki kupewa kwasababu kadha wa kadha.

Haifai hivi,anaeomba humjui shida yake ikoje.Usimwangalie mtu kava nini,kapanda gari gani au ananukia mafuta gani.

Haja yake ni msaada kwako,kama unacho mpe, wewe huna hasara ila faida.Wala usitie dhana juu yake,ikiwa yeye si mkweli basi ni juu yake yeye na Mola wake.Wewe wajibu wako umetekeleza na thawabu zipo kwako.

3.Kutembelea jamaa zako.

4.Kutembelea wagonjwa.

5.Kufutarisha watu – ( zaidi maskini wasio na uwezo )

6.Kusoma Quraan sana na kukithirisha dhikr na dua.

7.Kuhudhuria mihadhara na vikao vya dini baada ya sala.

8.Kujitahidi kufika mapema msikiti kila kabla ya sala ya jamaa.

Na mengi mengine ambayo tunayajua yenye kheri na fadhila kubwa kwa Allah tujitahidi kuyafanya.

Na vile vile tujiepushe na mambo ambayo yanabatilisha funga zetu kama:-

1.Kusengenya – tujiepushe na vikao na muzungumzo yasio na maana.

2.Kusema uongo.

3.Kutukana.

4.Kugombana na kugombanisha watu.

5.Kuangalia filamu

6.Kupoteza wakati kwa michezo.

7.Kuangalia yalioharamishwa.

Na mengineyo ambayo tunayaelewa.

Tunamuomba Allah (s.w.t) atujaalie wenye kuneemeka na rehma na barka zote za mwezi huu mtukufu kwa kujipinda kufanya ibada kwa wingi na kwa ikhlasi.

Na kutuepusha na yale yote yatakayotupotezea muda wetu kwa ajili ya kumfuata Sheitani mlaanifu,

Ameeeen.,,,,,


0 comments