Wednesday, 21 August 2013

MABILIONI YAKWAPULIWA SERIKALINI

Na Shehe Semtawa : TANZANIA DAIMA

KUNA ubadhirifu mkubwa unaofanywa na watendaji waandamizi wa serikali, kiasi cha kusababisha upotevu wa mabilioni ya fedha za umma.

Wakati Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa chini ya Waziri Bernard Membe ikisulubiwa jana kwa tuhuma za matumizi ya mabilioni ya fedha zisizo na maelezo, Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi nayo, inadaiwa kukabiliwa na uozo wa kutisha.

Hata hivyo, Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) ndiyo inayodaiwa kuwa kinara wa ubadhirifu wa fedha za umma, kiasi cha kumlazimu Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA, Zitto Kabwe kukiri kuwa uozo ndani ya serikali unatisha.

“Inaonyesha serikali kuu ina masuala mengi sana ya ubadhirifu ambayo Kamati ya PAC ilikuwa inaficha umma. Toka nimeanza kuwa Mwenyekiti PAC (Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali Kuu) sijaona wizara hata moja yenye afadhali.

“Leo wizara mbili tumezirudisha, hesabu zao madudu matupu. Wizara ya Ardhi na Wizara ya Mambo ya Nje ambayo hata BOQ ya jengo la JK Nyerere Convention hawana na ni mkopo kutoka China. Tutalipa kiasi gani sasa?” alisema Zitto jana mara baada ya kukutana na watendaji wa wizara hizo.

Uzito wa tuhuma za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, zimeisukuma PAC kumwomba Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh kuifanya ukaguzi maalumu baada ya kubaini madudu mengi.

Mwenyekiti wa muda wa kamati hiyo, Gaudence Kayombo alibainisha hayo jana, akidai kuwepo kwa matumizi makubwa ya fedha katika mikutano inayohusu wizara hiyo nje ya bajeti.

Mbali na matumizi ya mikutano ya wizara, Kayombo alibainisha kuwepo kwa tuhuma nzito za matumizi makubwa na yasiyoeleweka katika mradi wa ujenzi wa jengo kubwa la kisasa la Saramath lililopo ndani ya Uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere.

“Tunataka kujua jengo hilo lilijengwa kwa shilingi ngapi, na Wachina walitoa kiasi gani, maana tunaona kuna ukiukwaji mkubwa wa taratibu nyingi,” alisema Kayombo.

Aliongeza kuwa kamati yake imebaini matumizi mabaya ya fedha, hasa katika mikutano inayofanywa na wizara hiyo, hivyo wamemuandikia barua Utouh ili afanye uchunguzi.

Alisema kamati hiyo pia imebaini kuwepo kwa madeni makubwa yanayofikia kiasi cha sh bilioni 13 yanayodaiwa na wafanyakazi pamoja na wazabuni wa ndani.

Jijini Dar es Salaam, Kamati ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) imeshitushwa na upotevu wa zaidi ya sh bilioni mbili zilizotolewa kwa ajili ya miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa barabara katika Manispaa ya Ilala, na hivyo kukataa taarifa ya mwaka 2012 na 2013.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Dk. Hamisi Kigwangala wakati akitoa majumuisho ya ziara yao ya kutembelea miradi mbalimbali ya halmashauri hiyo, alishikwa na mshangao baada ya viongozi wa halmashauri hiyo kushindwa kuonyesha mchanganuo mzima wa matumizi ya fedha hizo.

Miradi ya barabara zote za halmashauri hiyo ilitengewa zaidi ya sh bilioni 13.6, hata hivyo fedha iliyotumika ni sh bilioni 11.7 huku zaidi ya sh bilioni 1 hazijulikani zilikokwenda.

Dk. Kigwangwala pia aliitaja miradi mingine ambayo matumizi ya fedha zake hazikueleweka zimetumikaje kuwa ilikuwa ni ujenzi wa barabara ya Magole na wa vitabu.

Aliongeza hata ile miradi ya viporo taarifa hazionyeshi kama imekamilika. Wameshindwa kabisa kufuata mfumo unaotolewa na halmashauri nyingine nchini.

“Taarifa yenu yote inaonyesha ni ya kukopi na kupesti, hivyo kamati inawaagiza mkajifunze tena jinsi ya kuandaa taarifa,” alisema.

Hata hivyo kamati hiyo imekiri kuwa kuna mgogoro mkubwa kati ya Mkurugenzi Mwendahasara Maganga na Meya wa Halmashauri hiyo, Jerry Silaa, kiasi cha kuathiri uendeshaji wa kazi za maendeleo kwa ajili ya wananchi.


Vinara 70 wa ubadhirifu kutajwa



Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Kamati za Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), Rajab Mbaruku amedai kuwa atawataja wakurugenzi 70 ambao ni vinara wa ubadhirifu wa fedha za umma nchini.

Akizungumza jana na waandishi wa habari baada ya kumalizika kwa kikao cha watendaji wa Halmashaji ya Jiji la Arusha, Mbaruku alisema atawataja wakurugenzi hao baada ya kubaini uwepo wa ushirikiano mkubwa wa ufisadi baina ya halmashauri, TAMISEMI na Hazina.

“Nitawataja hao wakurugenzi maana kuna kulindana…utakuta mkurugenzi katolewa Jiji la Mwanza na kuletwa Dar es Salaam wakati kule alikotoka kaacha ubadhirifu hii inaonyesha jinsi wanavyolindana,” alisema.

Mbaruku alisema kutokana na kulindana, kamati yake imekuwa inakutana na vikwazo vikubwa wakati wa kutembelea halmashauri. “Maana Tamisemi ikibaini tu kamati inatembelea halmashauri wanaandaa uhamisho kwa mkurugenzi na mwekahazina wa halmashauri hiyo,” alisema.

Alisema kuwa kamati imeamua kukutana na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Hawa Ghasia na Agrey Mwanri ili kujadiliana nao juu ya vikwazo wanavyokutana navyo.

Mbali na hilo, Mbaruku aliitaja Halmashauri ya Monduli jijini Arusha kuwa kati ya halmashauri inayofanya vibaya kwa miaka mitano mfululizo, huku jiji la Arusha nalo likituhumiwa kwa ubadhirifu wa hali ya juu na matumizi mabaya ya fedha.

0 comments