Saturday, 31 August 2013

VYUO VIKUU VIANAUKTA WA WANAFUNZI

Na Julieth Mkireri, Pwani, TANAZANIA DAIMA

 VYUO vikuu vya serikali nchini vinakabiliwa na upungufu wa wanafunzi 30,000.

 Upungufu huo umetokana na idadi kubwa ya ongezeko la vyuo huku kukiwepo na changamoto ya ufaulu hafifu wa wanafunzi wanaofikia kiwango cha kukidhi sifa za kujiunga na vyuo hivyo.

 Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa, alieleza hayo jana wakati wa ufunguzi wa vyumba vitatu vya madarasa ya Shule ya Sekondari Bwawani, wilaya ya Bagamoyo, mkoani Pwani, yaliyofunguliwa kwenye mbio za Mwenge mkoani hapa.

 Dk. Kawambwa ambaye pia ni mbunge wa Bagamoyo, alisema mbali ya changamoto ya uhaba wa wanafunzi vyuoni, pia baadhi ya shule za sekondari zina ukosefu wa madarasa ya kidato cha tano na cha sita.
Alisema ili kukidhi mahitaji ya vyuo vilivyopo wanafunzi wanatakiwa kuongeza jitihada katika masomo yao. Alitoa wito kwa wazazi kufuatilia maendeleo ya kimasomo ya watoto wao pindi watokapo shuleni na wawapo majumbani, ili kuongeza ufaulu kwa wanafunzi.

 Awali akipokea mwenge huo kutoka mkoa wa Morogoro, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mwantumu Mahiza, alisema miradi 65 ya maendeleo yenye thamani ya sh bilioni 6.5, ambapo miradi 19 itawekwa mawe ya msingi, 17 itazinduliwa na miradi 15 itafunguliwa na miradi 14 itakaguliwa na Mwenge huo.

0 comments