Wednesday, 11 September 2013

DARASA LA PILI KUPIGA TAIFA

MTIHANI mpya wa Taifa utaanzishwa kwa wanafunzi wa darasa la pili nchi nzima, ili kuchuja watakaoshindwa kusoma, kuandika na kuhesabu. Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo, alisema hayo jana akitangaza kuanza kwa mtihani wa Taifa wa kumaliza elimu ya msingi Tanzania Bara.

Mtihani huo wa kumaliza elimu ya msingi unatarajiwa kufanyika kesho na keshokutwa na kuhusisha watahiniwa 868,030 waliosajiliwa.

Akifafanua uamuzi wa kuanzishwa mtihani wa Taifa wa darasa la pili, Mulugo alisema mtihani huo ni sehemu ya utekelezaji wa mkakati wa matokeo makubwa sasa katika sekta ya elimu.

Malengo ya mtihani huo kwa mujibu wa Mulugo ni kuondoa uwezekano wa kuwa na wanafunzi katika madarasa ya juu, wasiojua kusoma, kuandika na kuhesabu na ili kufikia malengo hayo, watakaoshindwa mtihani huo, watarudia mpaka wajue kusoma na kuandika.

Aprili mwaka jana, Mulugo alipokuwa akizungumza na wafanyakazi wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), alikaririwa akikiri kuwa katika mtihani wa Taifa wa kumaliza elimu ya msingi wa mwaka juzi, kulikuwa na wanafunzi wasiojua kusoma, kuandika na kuhesabu, waliochaguliwa kujiunga na sekondari.

Kutokana na udanganyifu katika mitihani ya Taifa, Mulugo alikaririwa akiagiza wanafunzi walioingia kidato cha kwanza wapimwe uwezo wao wa kusoma na kuandika na kuhesabu.

Alikaririwa akisema kwa mujibu wa tathmini, mkoa wa Kilimanjaro uliongoza kwa kuwa na wanafunzi wengi wasiojua kusoma, kuandika na kuhesabu. "Mkoa wa Kilimanjaro una wanafunzi wasiojua kusoma na kuandika wapatao 660, Tanga 490 na Dar es Salaam 208," alikaririwa Mulugo bila kutaja matokeo ya mikoa mengine.

“Hili ndilo janga la kitaifa sasa. Si hayo mengine ambayo watu wanasema ni majanga ya kitaifa. Lazima tujiulize kwa nini watoto wanamaliza darasa la saba wakiwa hawajui kusoma na kuandika na wanafaulu?” Alihoji na kuongeza:

“Je, siku hizi hakuna tena somo la kusoma na kuandika? Kwa nini mtoto amalize shule bila kuwa na maarifa ya KKK (Kusoma, Kuandika na Kuhesabu)?

“Jambo la kusikitisha kuna mpaka baadhi ya wanafunzi wa kidato cha tatu, ambao hawajui kusoma wala kuandika. Tulipofikia si pazuri hata kidogo, lazima tuwe makini jamani.

“Tuheshimu Baraza la Taifa la Mitihani (Necta), tupate ufumbuzi wa mambo haya, Taifa hili ni letu sote, lazima tuhakikishe linasimama imara,” alikaririwa Mulugo.

Akitangaza kuanza kwa mtihani wa darasa la saba kesho, Mulugo alisema kati ya watahiniwa wote, wasichana ni wengi ambao ni 455,925 sawa na asilimia 52.52 ya watahiniwa wote na wavulana ni 412,105 sawa na asilimia 47.47. Masomo yatakayotahiniwa ni Kiswahili, Kiingereza, Sayansi, Hisabati na Maarifa ya Jamii.

Alisema wanafunzi 844,810 wanatarajiwa kufanya mtihani huo kwa Kiswahili, kati yao wavulana ni 400,335 na wasichana 444,475. Wanafunzi 22,535, kati yao wavulana wakiwa 11,430 na wasichana 11,105, wanatarajiwa kufanya mtihani huo kwa Kiingereza ambao ndio walikuwa wakiitumia kujifunzia.

Wanafunzi wasioona waliosajiliwa kufanya mtihani huo ni 88 wakiwamo wavulana 56 na wasichana 32 ambapo pia watahaniwa 597 wenye uoni hafifu ambao huhitaji maandishi makubwa wanatarajiwa kufanya mtihani huo.

Mulugo alisema maandalizi yote kwa ajili ya mtihani huo yamekamilika ikiwa ni pamoja na kusambazwa kwa karatasi za mitihani, fomu maalumu za OMR za kujibia na nyaraka zote muhimu zinazohusu mtihani huo.

Alitoa mwito kwa maofisa elimu wote wa mikoa na halmashauri kuhakikisha utaratibu wote wa mitihani unazingatiwa ipasavyo ikiwa ni pamoja na mazingira kuwa salama na tulivu na kuzuia mianya inayoweza kusababisha udanganyifu.

Pia alitoa mwito kwa wasimamizi kufanya kazi yao kwa umakini na uadilifu wa hali ya juu kwa kuwa baadhi ya wasimamizi wamekuwa wakishiriki kusaidia watahiniwa kuibia kwenye mitihani yao, na kuonya atakayebainika atachukuliwa hatua kali za kisheria.

Wanafunzi watakaojihusisha na vitendo vyovyote vya udanganyifu wa mtihani, alisema watawafutiwa matokeo.

cNHANZO: haBARI LEO

0 comments