Monday, 7 October 2013

WANANCHI WAPINGA TOZO YA SIMU

WATANZANIA wameendelea kuipinga tozo mpya ya sh 1,000 kwa kila laini ya simu, ambayo ilipitishwa na Bunge hivi karibuni na kuzua mvutano mkubwa baina ya serikali, wananchi na makampuni ya simu.

Tayari serikali imeiandikia barua Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) kuyaagiza makampuni ya simu kutoza kodi hizo kuanzia Julai 30 mwaka huu, licha ya awali kuahidi kuitazama upya kodi hiyo bungeni.

Hivi karibuni kituo cha televisheni cha ITV kupitia kipindi chake cha Kipima Joto, kilikusanya maoni ya wananchi juu ya kodi hiyo, na asilimia 99 ya Watanzania walisema kodi hiyo haiendani na uwezo wa kifedha wa watumiaji wa simu.

Ni asilimia 0.6 ya waliotoa maoni walisema ni sahihi kutoza kodi hiyo wakati asilimia 0.1 hawakuwa na upande wowote.

Watumiaji wa simu wapatao 700,000 wa mitandao mbalimbali ya simu walisema tozo ya kodi hiyi si sahihi kwa kuwa watumiaji wa huduma za mawasiliano nchini tayari wanalipa asilimia 14.5 ya matumizi yao ya simu kama kodi.

Wananchi hao kupitia maoni yao katika vituo vya ITV na Radio One waliishauri serikali kutafuta vyanzo mbadala vya mapato badala ya kuwatwisha mzigo mkubwa wa kodi watumiaji wa simu.

Hivi karibuni, Taasisi ya Watumiaji wa Bidhaa na Huduma ilifungua kesi Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kupinga sheria hiyo.

Pia makampuni ya simu ya Tigo, Airtel, Zantel, Vodacom Tanzania na Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) ambayo ni wanachama wa muungano wa makampuni yanayotoa huduma za simu za mkononi (MOAT) yalipinga kodi hiyo na kuiomba serikali itafute njia mbadala.

Taarifa za makampuni hayo zilibainisha kuwa watumiaji wa simu za mkononi wapatao milioni nane wanatumia chini ya sh 1,000 kwa mwezi na hawana uwezo wa kulipa kodi ya laini ya kila mwezi.


SOURCE: TANZANIA DAIMA

0 comments