Inawezekana kuwa na magari yasiyokuwa na dereva? Kampuni ya
mawasiliano ya kompyuta ya Google inasema ndiyo. Magari hayo yapo na
yataongozwa kwa kutumia kompyuta pekee, huku yakiwa na uwezo mkubwa wa
kuepuka au kutosababisha ajali barabarani.
Wanasayansi wa Google wanaosimamia teknolojia hiyo
mpya, wanaamini kwamba madereva wanafanya makosa mengi wawapo
barabarani, yakiwepo ya kizembe ama bahati mbaya na ndiyo yanakuwa
chanzo cha ajali mbaya barabarani.
Wakati teknolojia ya kompyuta ilipogundulika,
wanasayansi walisema wamegundua mbinu ya kufuta makosa ya kibinadamu
katika shughuli za hesabu.
Waliamini kuwa kila hesabu 500 afanyazo mtu ambaye
ni mtaalamu wa fani hiyo, lazima kuwepo na makosa yasiyopungua mawili.
Lakini baada ya kugundua kompyuta, maelfu kwa maelfu ya hesabu yanaweza
kufanyika bila makosa.
Makosa hayo ya kibinadamu yanayoweza kufanywa na
mtu bila kukusudia, ndiyo yanayoaminika kuweza kufanywa na dereva yeyote
akiwa barabarani.
Magari hayo yako je?
Mtaalamu wa kompyuta katika Chuo Kikuu cha
Stanford, Profesa Sebastian Thrun, anayesimamia, teknolojia hiyo
akisaidiana na mhandisi wa kampuni ya Google, Chris Urmson, wanasema
teknolojia hiyo itasaidia kuepusha ajali, foleni na pia kupunguza
kiwango cha mafuta yanayopotea kutokana na uendeshaji usiofaa.
Mhandisi Urmson anasema magari hayo hayatakuwa na
tofauti kwa kiasi kikubwa na mwonekano au miundo ya magari yaliyopo
sasa. Kama haitoshi yana chaguo la ama liendeshwe kwa kompyuta ama na
dereva.
Mwonekano wake
Kimwonekano, magari hayo anayaelezea
yatatofautiana na mengine, kwa kuwa na kifaa maalumu juu ambacho
kinasaidia mawasiliano na kutambua maeneo.
Anasema kwenye mfumo wa kompyuta zitatumika
programu mbalimbali kama vile ya 3D, ambayo itasaidia kuliongoza gari
kulingana na ramani ya eneo.
“Hii ina maana kwamba magari yote yatakuwa
yanatumia ramani ambayo lazima iingizwe kwenye mfumo wake ili itambue
barabara itakazopita ili kufika aneo ambalo mhusika ama wahusika
wanataka” anasema.
Isitoshe anasema gari hiyo ina vihisi vinavyosaidia kutambua
njia ambayo linapaswa kupita, ili lisiingilie njia ya magari mengine.
Pia kutambua gari au mtembea kwa miguu anayekatiza mbele yake.
Vihisi hivyo ambavyo viko pande zote za gari;
mbele, ubavuni nyuma, chini na juu, vinaweza kulisaidia pia kufahamu
eneo la taa zinazooongoza magari na kutambua wakati wa kuruhusiwa
kupita.
Ili kuhakikisha kuwa ramani za maeneo husika
hazina matatizo, mhandisi huyo anasema Google watapaswa kutumia magari
yao kuinakilisha vyema kwenye mfumo ambao utakusanya takwimu mbalimbali
za maeneo husika.
Ina maana kwamba ili nchi kama Tanzania iweze
kutumia teknolojia ya magari hayo, ni lazima kampuni ya Google ilete
wataalamu wake nchini ili kuzisoma barabara ambazo magari hayo yatapita.
Ikitokea barabara ikaongezwa ama kubadilishwa
mfumo au muundo wake, basi itabidi na ramani ya gari hilo ibadilishwe
ili kuepuka makosa.
Mhandisi Urmson anasema kuwa hata kama itatokea
taa za barabara zimeruhusu gari hilo, akipita mtembea kwa miguu
kimakosa, gari hilo litambaini na kumuacha apite.
“Iwapo gari jingine la namna hiyo litatokeza
ghafla katika makutano ya barabara yasiyoongozwa na taa, gari za mfumo
huo zitatambuana, hivyo mojawapo litampisha mwenzake apite kwanza.
Gari hizo, anasema zina uwezo wa kutambua wapi
zitembee kwa kasi na wapi zipunguze mwendo. Pia zina uwezo wa kufuatilia
magari, watembea kwa miguu na hata vitu vingine vya hatari vilivyopo
karibu yake.
“Gari hizo zina uwezo wa kutoa ishara ya kuelekeza
magari mengine nini yafanye na hata kuelimisha mengine ambayo
yanaonekana yanataka kuvunja sheria,” anasema mhandisi Urmson na
kuongeza:
“Hii ni teknolojia ambayo katika siku zijazo
itafanya usafiri wa barabarani kuwa rahisi zaidi, wa starehe, haraka na
wenye ufanisi.”
Google inaamini ifikapo mwaka 2020, magari mengi yanayoendeshwa kwa kompyuta yatakuwa yanatumika hasa katika nchi zilizoendelea.
Kwa mfano nchini marekani magari hayo yameweza
kutembea katika miji yenye msongamano wa magari mengi na kutembea zaidi
ya kilomita 300,000 bila kusababisha ajali.
Waanzilishi wa teknolojia hiyo katika kampuni ya Google, ni Larry Page na Sergey Brin.
CHANZO: MWANANCHI
CHANZO: MWANANCHI



0 comments