BAADHI ya wakazi wa Kibaha, mkoani Pwani, wanailalamikia Kampuni ya
Informal Sector Workers Union ya jijini Dar es Salaam kwa madai ya
kuwatapeli sh milioni 8.8.
Wakizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana, wakazi hao
walisema lengo lilikuwa ni kutaka kukopa pikipiki na wengine fedha,
lakini hadi sasa zoezi hilo halijafanikiwa na hawaoni dalili za kupata
mikopo.
Baadhi ya walalamikaji hao; Loyce Isack, Goodluck Marika na Emmanuel
Mhina ambaye ni mchungaji wa Kanisa la Pentekoste lililopo Mwanalugali,
walisema mgogoro kati yao na kampuni hiyo utaisha endapo watatimiziwa
mahitaji yao.
Walisema Machi mwaka jana walipata taarifa ya kuwepo kwa kampuni hiyo
katika ofisi ya CCM Wilaya ya Kibaha Mjini ikitoa mikopo ya fedha na
pikipiki na ndipo walipokwenda kujiunga kwa kufuata utaratibu
walioelezwa, lakini hadi sasa hakuna mikopo iliyotolewa.
Walieleza moja ya taratibu walizotakiwa kufanya ni kuweka dhamana ya
sh 650,000 na 500,000 pamoja na bima ya sh 38,000 ili wapate pikipiki
na ya fedha na kwamba marejesho yalikuwa yawe sh 56,500 kila wiki ndani
ya miezi sita.
Hata hivyo, pamoja na kufuata taratibu walizopewa pamoja na kutoa
fedha hizo, hakuna mkopo wa fedha wala pikipiki walizopata hadi sasa
licha ya kuwepo kwa juhudi za kufuatilia haki zao bila mafanikio.
Walisema wameshapeleka malalamiko hayo katika ofisi za Makao Makuu ya
Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani na kufungua jalada la uchunguzi lenye
namba RCO/PE/No 8/2013.
Walieleza hawakuwa na wasiwasi kwa kuwa kampuni hiyo ilikuwa ipo
ndani ya jengo la CCM, hivyo waliamini ilikuwa na lengo la kuwasaidia
wananchi wake.
Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Dauda Salmin, alitafutwa kupitia simu
yake ya kiganjani na baada ya kupokea na kusikia mwandishi akieleza
kuhusiana na jambo hilo alikata simu na kuzima.
CHANZO: TANZANIA DAIMA



0 comments