Sunday, 9 February 2014

MAHUJAJI 15 WA UMRAH WAFARIKI KWA MOTO HOTELINI MADINA




Watu wasiopungua 15 wamepoteza maisha na wengine 130 kujeruhiwa baada ya hoteli moja kuteketea kwa moto katika mji mtakatifu wa Madina nchini Saudi Arabia.

Vyombo vya habari vya Saudia vimesema hoteli hiyo ilikuwa na wageni 700 ambao walikuwa mjini Madina kwa ajili ya ibada ya Umrah. Imearifiwa kuwa wengi walikuwa ni raia kutoka mataifa mbalimbali wengi wakiwa Wamisri na Waturuki. 

Moto huo ulianza saa nane na dakika 33 Ijumaa usiku na kuendelea hadi mapema Jumamosi.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Misri imesema raia wa nchi hiyo ni kati ya waliopoteza maisha katika moto huo. Balozi wa Misri Afifi Abdel- Wahab alinukuliwa akisema kwamba Wamisri 15 walikufa katika moto huo.

Baadhi ya majeruhi walitibiwa hapo hapo na wengine walipelekwa hospitali za King Fahd na Ansar. Wageni
wengi wamehamishiwa katika hoteli zingine mjini humo. 

Maafisa wa usalama mjini Madina wamesema uchunguzi umeanza ili kubaini chanzo cha moto huo.


CHANZO: AHBABUR RASUUL

0 comments