
Shirika la kutetea haki za binaadamu Human Rights Watch limetaka hatua za haraka zichukuliwe kwa lengo la kuzuia mauaji ya halaiki ya Waislamu huko Jamhuri ya Afrika ya Kati.
Mkuu wa masuala ya dharura katika shirika hilo Peter Bouckaert amesema Waislamu wanakabiliwa na mustakabali mgumu sana katika nchi hiyo ya kati mwa Afrika na hivyo kuna haja ya hatua za dharura kuchukuliwa ili kuzuia hali ya mambo kuwa mbaya zaidi.
Waislamu ni takribani asilimia 15 ya watu milioni 4.6 katika Jamhuri ya Afrika ya Kati. Ripoti zinasema kuwa magenge ya Wakristo wenye misimamo mikali wamewaua maelfu ya Waislamu nchini humo huku mamia ya maelfu wakilazimika kukimbilia katika nchi jirani.
Bouckaert ametoa wito wa kutumwa askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa huko Jamhuri ya Afrika ya Kati, 'la sivyo Waislamu hawatakuwa na mustakabali katika nchi hiyo.'
Afisa huyo amenukuliwa akisema kuwa Waislamu wametimuliwa kikamilifu katika baadhi ya mitaa katika mji mkuu wa nchi hiyo Bangui. Amesema kuna njama makusudi za kuhakikisha hakuna Mwislamu anayebakia mjini humo.
Aidha amesema misikiti imebomolewa na kwamba ameona msikiti moja tu katika mtaa ambao ulikuwa na misikiti nane mjini Bangui.
Kuna askari 1,600 wa Ufaransa na maelfu ya askari wengine wa kulinda amani kutoka nchi za Kiafrika huko Jamhuri ya Afrika ya Kati lakini wameshindwa kuzuia mauaji ya Waislamu yanayofanywa na magenge ya Wakristo.
CHANZO: AHBAABUR RASUL



0 comments