Thursday, 6 November 2014

SERIKALI YABAKIZA BIL 4/= TU DENI LA WALIMU

BUNGE limeelezwa kuwa deni la walimu linalodaiwa serikalini limeshuka hadi kufikia Sh bilioni 4 tu kutokana na mfumo mzuri wa ulipaji uliowekwa na Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).

Katika hatua nyingine, Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai amefikisha kilio cha wabunge kwa Waziri wa Fedha, Saada Salum Mkuya cha kutolipwa posho zao tangu walipokuwa katika vikao vya kamati jijini Dar es Salaam na sasa wakiwa Dodoma.

Akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalum, Diana Chilolo (CCM) kuhusu madai ya walimu, Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba alisema sasa kiwango hicho kimeshuka hadi kufikia Sh bilioni 4 tu, kutoka zaidi ya Sh bilioni 60 ambazo zilikuwa zinadaiwa.

Alisema hatua hiyo inadhihirisha nia njema ya serikali ya kulipa madeni yote ya walimu kwa lengo la kuboresha maisha yao na hasa baada ya kuboreshwa kwa mfumo wa ulipaji ambao sasa hautawezesha tena deni hilo kukua kama ilivyokuwa nyuma.

Awali akijibu swali la msingi la Mbunge wa Vunjo, Augustine Mrema (TLP) kuhusu mishahara ya walimu kulipwa na Hazina kupitia benki, Nchemba alisema mishahara ya watumishi wa serikali hulipwa kupitia Benki ya NMB kwa watumishi walio nje ya Dar es Salaam na Benki ya CRDB kwa walioko Dar es Salaam.

Alisema lengo la serikali kulipa moja kwa moja kwenye akaunti za watumishi ni kuhakikisha udhibiti wa malipo ya mishahara hewa kwa watumishi wasiostahili.
Alisema ili kutekeleza utaratibu huo, waajiri wote walielekezwa kuhakikisha makato yote katika mishahara ya watumishi yanaingizwa kwenye orodha ya malipo ya mishahara kupitia Mfumo wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara (HCMIS).

Aidha alisema hakuna makato yoyote yanayoruhusiwa kufanyika katika mshahara wa utumishi pasipo kubainishwa kwenye orodha ya malipo na kupewa namba ya utambulisho ambayo hutolewa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma.

Katika hatua nyingine, Naibu Spika wa Bunge, Ndugai jana alisimama bungeni na kuulizwa swali alilodai kuwa ameagizwa na wabunge wengi akisema wabunge hawafahamu watalipwa lini malipo yao.

“Wabunge wanasema Waziri wa Fedha hausomeki tangu walipokuwa kwenye vikao Dar es Salaam na sasa wakiwa hapa Dodoma, kwa hiyo Waziri unatakiwa kufanya jambo fulani kwa wabunge,” alisema Ndugai.


CHANZO: HABARI LEO

0 comments