Mashindano hayo yanatarajiwa kufanyika Desemba 14, mwaka huu jijini London, Uingereza. Tayari Miss Tanzania 2013, Happiness Watimanywa ameshaondoka nchini Jumamosi iliyopita kwenda nchini humo kwa matayarisho.
Kwa mujibu wa barua pepe kutoka kwa Mwenyekiti wa Miss World, Julia Morley kwenda kwa mwanzilishi wa Miss Tanzania, Prashant Patel na Mkurugenzi wa Lino International Agency, Hashim Lundenga iliyotumwa Jumapili iliyopita, Tanzania haijalipa ada hiyo.
Katika barua hiyo kiongozi huyo anasema: “Nimejulishwa kuwa bado ada yenu ya ushiriki haijalipwa. Itakuwa vyema kama suala hili litashughulikiwa haraka iwezekanavyo”.
“Hii itakuwa aibu kubwa kwa taifa,” alisema Patel na kuongeza kuwa pia uwezekano wa kufutwa kwa leseni ya Lino ni mkubwa. Imefahamika kuwa Lino International Agency imekuwa na deni linalofikia Pauni za Uingereza 30,000 katika kipindi cha miaka sita iliyopita na kuwa leseni ya kutayarisha shindano hilo mwaka huu ilitolewa kwa masharti ya kuanza kupunguza deni hilo.
Mwisho wa kulipa ada ili Tanzania ishiriki mwaka huu ilikuwa Septemba 30, mwaka huu. Kwa mujibu wa Patel, Lundenga alikuwa ameahidi kulipa ada hiyo pamoja na kuanza kupunguza deni hilo kwa muda uliokubaliwa, jambo ambalo inaonekana halijatekelezwa hadi sasa.
Akilizungumzia hilo jana, Lundenga alisema hana taarifa kuhusu barua pepe hiyo na kwamba aliwasiliana na Miss World mara ya mwisho Oktoba 2 mwaka huu.
Kuhusu kudaiwa, Lundenga alikiri kuwa na deni na kusema kuwa hiyo ni kati ya kampuni mbili, Lino Agency na Miss World.
“Yeye Patel anazungumza hili kama nani, yeye kanipeleka mahakamani kesi yetu ipo huko, sasa mambo mengine anayatakia nini? Kudaiwa ndio nadaiwa lakini sio ajabu hata serikali inadaiwa itakuwa mimi? Lakini jambo hili ni kati ya kampuni mbili, Lino na Miss World, yeye (Patel) amenipeleka mahakamani sasa anataka huruma ya vyombo vya habari ama nini? Tukutane huko,” alisema Lundenga.
Pamekuwa na msukosuko wa Miss Tanzania mwaka huu, baada ya mshindi Sitti Mtemvu kujiuzulu kwa kashfa iliyokuwa inamuandama ya kudanganya umri wake na taji kupewa aliyeshika nafasi ya pili, Lilian Kamazima.
Suala la Mtemvu kudaiwa kudanganya umri lipo kwenye vyombo vya sheria kwa sasa kwa uchunguzi.
Pia Patel amemburuza aliyekuwa mshirika wake, Lundenga kwa kukiuka makubaliano ya jinsi ya kuendesha mashindano hayo nchini. Bado kesi hiyo inaendelea kusikilizwa.
CHANZO: HABARI LEO



0 comments