Tuesday 23 December 2014

TIBAIJUKA AFUTWA KAZI

By    


Kashfa ya uchotwaji wa fedha za akaunti ya Escrow imemwondoa kigogo wa pili baada ya jana Rais Kikwete kutangaza kwamba atateua mtu mwingine kuchukua nafasi ya Waziri wa ardhi,nyumba na maendeleo Makazi Prof. Anna Tibaijuka.

Tibaijuka anakua kiongozi wa pili mwandamizi wa Serikali kuondoka madarakani kwa kashfa hiyo baada ya mwanasheria mkuu Jaji Fredrick Werema kujiuzulu hivi karibuni.

Aidha hatua hiyo inakuja baada ya hivi katibuni Tibaijuka kuitisha mkutano na waandishi wa habari na kusema hawezi kujiuzulu kwa kuwa alichukua bilioni 1.6 kwa nia njema kutoka kwa James Rugemalira wa VIP Engeneering na kwamba akifanya hivyo hadi Rais atamshangaa.

Akiwahutubia wazee wa Jijini Dar es salaam Kikwete alisema ‘Tumemuulizi Tibaijuka fedha hizo nyingi amezipata vipi?akatujibu kwamba ni kwa ajili ya kuendesha shule,bodi ya shule nayo ikatetea kwamba na shule ikatetea kwamba ni fedha za shule na hiyo kwetu haina tatizo kusaidia shule,sisi hatukua na tatizo kwa nini shule imepewa fedha tatizo lilikua kwanini fedha zimeingia kwenye akaunti yake badala ya akaunti ya shule? alitujibu kuwa hayo ndiyo masharti aliyopewa na Rugemarila…alisema Kikwete.

“Tukaona kwamba ,hapa kuna mapungufu,tukakubaliana na tukamwomba atuachie nafasi ili tumteue Waziri mwingine”Aliongeza.

TUJIKUMBUSHE KAULI YA JEMBE ANNA TIBAIJUKA ILIVYOKUA

WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, wa wakati huo Profesa Anna Tibaijuka, aliwahi kusema hatojiuzulu kwa sababu kufanya hivyo si fasheni.

Pamoja na kauli hiyo, pia aliweka bayana kuwa yeye na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, bado wanategemewa na Rais Jakaya Kikwete katika kumsaidia kufanya kazi.

Kauli ya Profesa Tibaijuka ilitoka siku chache baada ya kujiuzulu kwa aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema kutokana na kashfa ya uchotwaji wa zaidi ya Sh bilioni 300 katika Akauti ya Tegeta Escrow iliyokuwa imefunguliwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Mbali na hayo, waziri huyo alieleza endapo uchunguzi utafanywa na kubaini fedha ambazo ziliingizwa kwenye akaunti yake na mmiliki wa Kampuni ya VIP Engineering, James Rugemalira si halali, basi yupo tayari kuzirudisha.

Prof Tibaijuka alizungumzia kuhusu kuhusishwa kwake na sakata la Akaunti ya Escrow, Profesa Tibaijuka alisema wanaodhani kwamba anatarajia kujiuzulu wanakosea kwani kufanya hivyo si kutenda haki katika dhana ya maendeleo.

Profesa Tibaijuka alisema anavishangaa baadhi ya vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kwa kumwita ‘Mama Escrow’ huku akiweka wazi na kujiita yeye ni ‘mama wa migogoro ya ardhi’ na si ‘mama wa migogoro ya Escrow’.

“Mlifikiri nimekuja kujiuzulu, kumbe ndiyo maana mmekuja wengi, sikuja kujiuzulu ng’o kwani sina kosa na siwezi kujiuzulu kwa ajili ya mchango wa shule. Nikijiuzulu nitakuwa sitendi haki katika dhana ya maendeleo na kujiuzulu siyo fasheni.

“Sijaja kujiuzulu wala kutetea watu wenye madhambi, pia uongo ukirudiwa mara nyingi unageuka kuwa ukweli, kilichonileta hapa ni kufafanua lengo la fedha hizo ambazo zilikuwa za shule ingawa suala lenyewe linaonekana kuwa na utata.

“Fedha hizo zilitolewa na watu wenye nia njema ya elimu kwa watoto wa kike kwani kipindi hicho elimu yao ilikuwa katika kiwango cha chini tofauti na wavulana hali iliyoleta mvutano kuwa watafutiwe kiwango maalumu cha ufaulu.

“Wizi na uongo ni dhambi, tusiwe watu wa kuhukumu kwani ni dhambi ya mauti, sikuwahi kuitwa na Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali inayoongozwa na Zitto Kabwe wala kamati yoyote kueleza suala hilo na nilishangaa kuona jina langu lipo kwenye orodha ya Escrow,” alisema Profesa Tibaijuka.

Katika mkutano huo, Tibaijuka alisisitiza kuwa anaona fahari kufanikisha mchango wa shule yake iliyoingiziwa fedha hizo, na kwamba aliyemfadhili aliweka masharti ya kufungua akaunti Benki ya Mkombozi pekee na kisha kuingiziwa kiasi cha Sh bilioni 1.617. Aidha alisema maazimio yaliyotolewa na Bunge ya kutaka uchunguzi uendelee kufanyika, bado yamekuwa yakileta mkanganyiko kwani azimio namba tatu linataka waliohusika wawajibishwe.

“Nikijiuzulu hata Rais Jakaya Kikwete atanishangaa kwani fedha nilizopata ni za shule na kwa ajili kukomboa elimu nchini, hasa kwa watoto wa kike kutokana na wazazi wengi kutoweza kumudu gharama za shule,’’ alisema.Matokeo ya mkutano wa jana Raisi alipozungumza na wazee wa Dar-Es-Salaam na wilaya zake, alimfuta kazi Anna Tibaijuka.

Desemba 16, mwaka huu aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema ambaye ni mmoja wa watuhumiwa katika kashfa ya Escrow alitangaza kujiuzulu.

Hatua hiyo ya Werema ilikuja wakati Watanzania wakiwa bado wanasubiri uamuzi wa Rais Kikwete kuhusu maamizio nane ya Bunge yaliyotokana na Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), aliyekagua miamala ya Akaunti ya Tegeta Escrow.

Katika maazimio ya Bunge, baadhi ya viongozi ambao chombo hicho kiliona wana makosa na kutaka mamlaka zao za uteuzi ziwachukulie hatua, ni Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Muhongo, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Tibaujuka, Jaji Werema, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini Eliakim Maswi na wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Tanesco.


CHANZO: BBC SWAHILI

0 comments