Mtendaji Mkuu wa TANROADS Patrick Mfugale |
Mkutano huo umeshirikisha wahandisi , wanasheria na wawakilishi kutoka Wizara ya Ujenzi, Wizara ya Fedha na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Akifungua mkutano huo jana jijini Dar es Salaam, Mtendaji Mkuu wa Tanroads, Patrick Mfugale alisema mradi huo utatekelezwa kwa ushirikiano baina ya Serikali na Sekta binafsi (PPP).
Andiko linaloandaliwa na Kampuni ya Ushauri M/S Cheil Engeneering ya Korea, linatarajiwa kukamilika Agosti mwaka huu na litatumika kuingia mkataba kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa mradi.
Alisema andiko litakuwa ni kielelezo cha kusaidia Serikali kujipanga ni jinsi gani itashirikiana na sekta binafsi katika miradi mbalimbali ya barabara, ambapo mkutano huo utawapa wadau hao nafasi ya kupendekeza nini kiwepo na kisiwepo katika andiko hilo.
“Andiko hilo litasaidia kuonyesha madhara ya kimazingira, fedha zinazohitajika, masuala ya sheria na mahitaji yote ambayo yatatakiwa katika utekelezaji wa mradi wakati ukifika,” alisema.
Kwa mujibu wake, utafiti uliofanyika mwaka 2011, ulionesha barabara ya Dar es Salaam hadi Chalinze inapitisha zaidi ya magari 67,000 kwa siku hivyo ikifika 2017 hali itakuwa mbaya zaidi.
Alisema utekelezaji wa mradi huo hautagusa barabara iliyopo na itakapokamilika itakuwa ikilipiwa, hivyo ambao hawatakuwa na uwezo watalazimika kuendelea kutumia barabara hiyo ya zamani na ndiyo sababu Serikali imeamua kushirikisha sekta binafsi.
Kamishna wa Sekta Binafsi Wizara ya Fedha, Dk Frank Mhilu akiwasilisha ripoti ya awali alisema Serikali inajipanga kuhakikisha kwamba mradi wa ujenzi wa barabara hiyo unakamilika kwa wakati pindi utakapoanza kutekelezwa.
CHANZO: HABARI LEO
0 comments