Zitto Kabwe kutoka Facebook
"Nimalizie kwa stori yangu. Nilizaliwa katika umasikini wa kutisha kama Watanzania wengi wa vijijini. Nimekwenda shuleni bila viatu na wakati mwingi tumbo likiwa tupu ama nimekunywa uji wa unga wa Yanga uliotiwa chumvi.
Darasani nilikuwa ninasoma na watoto wa watu wote wenye mamlaka pale mjini Kigoma. Wote tulikuwa tunafundishwa na Mwalimu huyo huyo na tunakaa darasa hilo hilo, tunapata elimu hiyo hiyo. Leo mimi ni msomi mwenye shahada ya Uzamili [......].
Wenzangu wengi pia wanaendesha maisha yao na wengine wapo hapa Marekani wakitafuta maisha.
Leo mtoto wa masikini Tanzania hapati elimu anayopata mtoto wa mwenye uwezo. Mtoto wa masikini hakutani na mtoto wa mwenye uwezo. Wanasoma shule tofauti. Wanafundishwa na walimu tofauti.
Hawachezi pamoja. Wote wakimaliza kidato cha Sita, mtoto wa mwenye uwezo ana nafasi kubwa zaidi ya kupata mkopo kwenda Chuo Kikuu kwa sababu amesoma shule bora zaidi hivyo anapata daraja kubwa zaidi la kupewa mkopo na Bodi ya Mikopo.
Wakati nasoma, kikwazo kilikuwa uwezo wako tu kichwani. Hivi sasa kikwazo ni kipato pia. Tofauti ya kipato nchini ni kubwa lakini sisi wanasiasa hatuioni.
Wakati wenzetu wanajiandaa kufaidika na ‘demographic dividend’ kwani watoto wao wanapata elimu bora, sisi hata hatujiandai na ‘demographic Bomb’ litakaloletwa na kundi kubwa la vijana wasio na elimu wala ujuzi.
Shiriki kurejesha Tanzania yenye kutoa fursa kwa kila raia bila kujali hali yake ya kipato. Shirika kurejesha Tanzania yenye Usawa kwenye fursa na yenye demokrasia."
Nukuu ya moja ya hotuba yangu mwaka 2012
0 comments