NAIBU Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Juma Nkamia amewataka wamiliki wa viwanja na ukumbi wa Klabu ya Leaders katika Manispaa ya Kinondoni, Dar es Salaam kufuata taratibu katika uendeshaji wake, ikiwa ni pamoja na kuacha kupiga muziki nyakati za usiku.
Nkamia alitoa agizo hilo jana bungeni kwa maelezo kuwa eneo hilo ni kwa ajili ya burudani nyakati za mchana kwa kuendesha michezo na mabonanza mbalimbali, lakini sio kupiga muziki nyakati za usiku kwani eneo hilo ni la wazi.
Alisema watoaji wa burudani katika viwanja hivyo wamekuwa wanavunja taratibu za matumizi kutokana na kupewa kibali cha kufanya hivyo na Manispaa ya Kinondoni, na kuonya kuwa sasa watachukua hatua kali kwa watakaokiuka sheria.
Leaders Club inamilikiwa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na ni maarufu jijini Dar es Salaam kutokana na kuendesha michezo mbalimbali na mabonanza ya taasisi malimbali za serikali na binafsi.
Hata hivyo, baadhi ya bendi zimekuwa zinapiga muziki katika eneo hilo nyakati za mchana na usiku pia.
Aidha, Nkamia pia amewataka wamiliki wa kumbi za starehe, mabaa na nyumba binafsi kufuata taratibu na sheria zilizowekwa kwa mujibu wa vibali na leseni walizopewa na mamlaka husika.
Nkamia alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Hilda Ngoye (CCM), aliyehoji mkakati wa Serikali katika kudhibiti usumbufu wa kumbi za starehe kwa wakazi jirani likiwemo eneo la Leaders Club.
Katika majibu yake, Nkamia pia alisema upigaji marufuku huo unalihusu pia klabu marufu ya Matei ya mjini hapa ambayo inapiga muziki usiku wakati iko eneo la wazi na imejengwa karibu na makazi ya watu.
Alisema jukumu pia la kila mwananchi kuchukua hatua kwa kutoa taarifa katika vyombo husika kuanzia ngazi ya Serikali za Mtaa, Kata, Polisi, Halmashauri za Wilaya, Basata pamoja na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya.
“Mwito wangu kwa wamiliki wa kumbi za starehe, mabaa a nyumba binafsi ni kuwakumbusha wafuate taratibu na sheria zilizowekwa kwa mujibu wa vibali na leseni walizopewa na mamlaka husika,” alisema Nkamia.
Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Dk Binilith Mahenge alisema wizara yake imeandaa kanuni za kelele na vitetemo kwa ajili ya kudhibiti upigaji wa muziki kwenye maeneo ya wazi ikiwemo baa, kumbi za starehe na makanisani. Alisema kanuni hizo ambazo zimekamilika kuchapishwa zitazinduliwa Aprili 13, mwaka huu.
Chanzo: habarileo.co.tz
0 comments