Monday 18 May 2015

RAISI WA MSUMBIJI AWAPA OFA TANZANIA YA KUTOLIPIA VIZA

Rais Filipe Nyusi wa Msumbiji (kushoto) akiwapungia wananchi waliojitokeza kumpokea wakati akiwasili Ikulu, Dar es Salaam jana kwa ziara rasmi ya siku tatu. (Picha na Yusuf Badi)
RAIA wa Tanzania na Msumbiji watakaotaka kuingia katika nchi hizo na kukaa wa miezi isiyozidi mitatu, hawatalipia viza kama ilivyokuwa awali, imeelezwa.

Aidha, imetangazwa pia kuwa, wanafunzi kutoka katika nchi hizo kuanzia sasa wanaruhusiwa kusoma kokote ndani ya Msumbiji na Tanzania wakitumia pasipoti zao zitakazogongwa viza bure, kwa kipindi chote cha masomo yao, hata kama ni miaka mingi.

Hatua hizo zimefikiwa Ikulu, Dar es Salaam jana baada ya Marais Jakaya Kikwete na Filipe Nyussi wa Msumbiji kukubaliana kufanyia marekebisho mkataba wa masuala ya uhamiaji kati ya nchi hizo mbili kudumisha udugu, urafiki na uhusiano wa kirafiki.

Makubaliano hayo yalifikiwa baada ya viongozi hao wakuu wa nchi hizo kufanya mazungumzo ya faragha kwa saa kadhaa Ikulu, na kisha Mawaziri; Jaime Basilio Monteiro, wa Mambo ya Ndani wa Msumbiji na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Tanzania, Bernard Membe, aliyemwakilisha Waziri wa Mambo ya ndani ya nchi, Mathias Chikawe, kusaini hati ya makubaliano hayo.

Mkataba huo wa sasa wenye marekebisho katika maeneo matatu makuu, umeeleza pia kuwa muda wa siku 30 uliokuwa ukitolewa na Msumbiji kwa watanzania, kukaa nchini humo bila kulipia viza sasa umeongezwa na kuwa siku 90.

Kutokana na matakwa mapya ya mkataba huo wa sasa, Membe alisema umeweka usawa wa siku za kuishi kwenye nchi hizo mbili kwa raia wa Tanzania na Msumbiji, tofauti na ilivyokuwa awali kwamba watanzania walipewa siku hizo kuwepo bure kwenye nchi hiyo wakati raia wa Msumbiji waliweza kuishi kwa siku 90 bila kutozwa ada ya viza.

“Makubaliano ya Marais hawa yameleta ahueni kubwa kwa raia wa nchi hizi mbili katika masuala ya uhamiaji. Wanafunzi nao wamepata nafuu kubwa kwa sababu hawataulizwa ada ya viza tena hadi wamalize masomo,” alisema Membe.

Aliongeza kuwa, mabadiliko hayo yanahusu hati za kidiplomasia, za kiserikali na za kawaida ambapo, mtumiaji atagongewa viza bure kwa siku atakazo kaa, ilimradi zisizidi 90.

Membe alieleza kuwa kabla ya makubaliano hayo, raia wa Msumbiji alipaswa kulipa ada ya viza ya Sh 10,000 tu, ili kukaa nchini kwa siku zisizo zidi 90, wakati raia wa Tanzania aliyekwenda Msumbiji na kukaa kwa zaidi ya siku 30, alipaswa kulipa Dola za Marekani 900 ikiwa ni ada ya viza.

Pia, alibainisha kuwa, Mtanzania aliyekwenda nchini humo kwa shughuli za biashara alipaswa kulipa ada ya viza ya Dola za Marekani 700, wakati mfanyabiashara wa Msumbiji aliyekuja nchini kwa shughuli kama hizo alitozwa ada ya viza ya Dola za Marekani 200 tu.

Rais Nyussi aliingia nchini saa 6:00 mchana kwa kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere na kulakiwa na mwenyeji wake, Rais Kikwete, kabla ya kwenda Hoteli ya Hyatt Regency Kilimanjaro kwa mapumziko mafupi na baadaye Ikulu kwa mazungumzo yaliyo zaa makubaliano hayo.

Akiwa uwanja wa ndege, Rais Nyussi alikagua gwaride la heshima, kupigiwa mizinga 21 na kujionea ngoma ya asili ijulikanayo kwa jina mnanda.


chanzo: habari leo

0 comments