Saturday 30 May 2015

TAMASHA LA KASWIDA KUFANYIKA DAR OKTOBA

TAMASHA la Kaswida linalotarajiwa kufanyika Dar es Salaam kesho, pia litatumika kuombea amani Taifa katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.

Kwa mujibu wa waandaaji wa tamasha hilo, ambalo mgeni rasmi atakuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, maandalizi muhimu yamekamilika, ambapo zaidi ya madrasa 50 zimethibitisha kushiriki.

Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya tamasha hilo litakalofanyika viwanja vya sekondari ya Benjamin Mkapa, Dar es Salaam jana, Ustaadhi Jumanne Ligopora ilieleza wana matumaini makubwa litafanikiwa.

“Huu ni mwaka wa Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani, hivyo tumekubaliana kutumia tamasha hilo kuomba dua maalumu kwa ajili ya amani ya Taifa letu.

“Tunaamini kila Mtanzania anapenda amani, hivyo tutamuomba Mungu atusaidie tupite salama katika kipindi hicho cha uchaguzi. “Waziri Membe amethibitisha kujumuika nasi, tunaomba na wadau wengine waje kwa wingi katika tukio hili kubwa, ” alisema Ustadhi Ligopora.

Alisema pia wamewaalika mashekhe mbalimbali kutoka mikoa ya Tanga, Pwani, Lindi, Morogoro na Dar es Salaam ili washiriki katika tukio hilo, ambalo ni mara ya kwanza kwa tamasha la namna hii kufanyika nchini.

Alifafanua kuwa tamasha hilo limeandaliwa na Ulamaa Promotions Centre na kwamba madrasa hizo baadhi ni za Dar es Salaam na nyingine zinatoka mikoa jirani na Dar es Salaam.

0 comments