Thursday, 22 October 2015

BAA ZA AMULIWA KUTOKUFUNGULIWA USIKU WA KUAMKIA UCHAGUZI

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki
Serikali jijini Dar es Salaam imeagiza baa zote zinazouza pombe mpaka asubuhi kusitisha shughuli hiyo mkesha wa siku ya uchaguzi ili kuimarisha usalama Jumapili ijayo.

Aidha, imesisitiza kwamba kila mwananchi atakayekwenda kupiga kura ahakikishe anarudi nyumbani baada ya shughuli hiyo badala ya kukaa katika vikundi kusubiri matokeo vituoni.

Agizo hilo lilitolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki, katika ibada maalum ya kuliombea Taifa amani na mvua, iliyoendeshwa na Askofu Charles Gadi wa Kanisa la Huduma ya Good News for All Ministry, jijini Dar es Salaam jana.

Askofu Gadi katika maombi yake alisisitiza suala la amani na kumuomba Mwenyezi Mungu alete mvua ili mabwawa yanayozalisha umeme yajae maji nishati ya umeme ipatikane nchini kwa uhakika.

 Katika ibada hiyo, Sadiki alisema ikiwa baa zitauza pombe mpaka asubuhi watu wengi wakiwamo vijana watashindwa kwenda kupiga kura ama watakwenda huko wakiwa wamelewa na baadhi yao kuishia kufanya fujo. “Nimeagiza wakurugenzi wa manispaa zote tatu za mkoa wa Dar es Salaam kuhakikisha wanasimamia agizo hili  la baa kufungwa mapema badala ya kukesha katika maeneo mbalimbali mkesha wa kuamkia siku ya upigaji kura,” alisema.

Alisema baadhi ya vijana ni walevi na ikiwa pombe zitauzwa mpaka asubuhi, watashindwa kwenda vituoni kupiga kura Jumapili ijayo. “Mimi huwa napita mitaa mbalimbali asubuhi nakuta vijana wengi wameshikilia bia asubuhi, sasa watu kama wale wanawezaje kwenda kupiga kura Jumapili ijayo kama baa zitakesha,” alisema.

Kwa upande wake, Askofu Gadi alisema amani ya nchi ndiyo msingi mkubwa wa maendeleo na kwamba ndiyo maana kila mara analiombea Taifa. Aliomba Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) kumtanguliza Mwenyezi Mungu wakati wa kusimamia  mchakato wa upigaji kura pamoja na kuzihesabu. Alisema ikiwa Nec haitatenda haki ambayo itaongozwa na Mungu, kunaweza kusababisha uvunjifu wa amani iliyopo na kwamba yeye kama kiongozi wa dini asingependa hilo litokee.

Askofu Gadi ni miongoni mwa maaskofu ambao wamekuwa wakifanya maombi kwa Taifa mara kwa mara ili kumuomba Mungu alijalie amani na neema, huku akishirikisha viongozi wa serikali.

CHANZO: NIPASHE.

0 comments