Thursday 22 October 2015

CHADEMA: TUKISHINDWA TUTAKUBALI MATOKEO

By    

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimesema kikishindwa kwa haki kitakubali matokeo. Kimeshauri wagombea wa vyama vya siasa nchini, vinavyoshiriki kwenye Uchaguzi Mkuu, kukubali matokeo ya kura ya kushinda au kushindwa kwa haki baada ya kura kuhesabiwa na kutangazwa mshindi.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Chadema, Reginald Munisi alisema ushauri huo unapaswa kuzingatiwa na vyama vyote, kama ambavyo mwangalizi wa kimataifa wa uchaguzi, aliyekuwa Rais wa Nigeria, Goodluck Jonathan alivyoshauri hapo juzi.

Munisi alisema ni vyema wagombea nafasi za urais na nyingine, wanapaswa kukubali matokeo ya kura, iwapo uchaguzi huo utafanyika kwa uhuru na haki ili kudumisha demokrasia nchini.

“Niwashauri wagombea wote wanaoshiriki uchaguzi huu utakaofanyika Jumapili hii (Oktoba 25) wazingatie ushauri wa aliyekuwa Rais wa Nigeria, Jonathan, watakaoshinda kwa haki washinde watakaoshindwa kwa haki nao wakubali,” alisema Munisi.

Alisema kwa upande wao, Chadema iwapo watashindwa kwa haki, watakubali matokeo. Akizungumzia mchakato wa maandalizi ya Uchaguzi Mkuu, unaofanyika Jumapili wiki hii, Munisi alisema wameiandikia barua Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kutaka ufafanuzi wa baadhi ya maelekezo yao ya ziada waliyotoa kwa wasimamizi wa uchaguzi.

Alisema katika maelekezo hayo, kuna suala la baadhi ya kadi ya mpigakura kuwa na namba tofauti na ile iliyo kwenye daftari la kudumu la mpigakura. Alisema kwamba watu hao, wataruhusiwa kupiga kura ili hali watu walio kwenye daftari hilo ila majina yao kama hayapo kwenye vituo vya kupigia kura, hawataruhusiwa kupiga kura.

Aidha, alisema wanataka ufafanuzi wa orodha ya majina yaliyoongezwa kwenye vituo vya kupigia kura.

Chanzo: Habari leo

0 comments