Rais Jakaya Kikwete akiwa na Rais Uhuru wa Kenya Ikulu mjini Nairobi. |
Rais Uhuru aliyasema hayo juzi mjini hapa, wakati wa dhifa ya kitaifa aliyomwandalia Rais Kikwete aliyekuwa hapa kwa ziara ya kiserikali ya siku tatu. “Tumekuwa marafiki wa muda mrefu, leo tunajisikia furaha kubwa kuagana na rafiki wa muda mrefu na mtu muhimu kwa Kenya.
Tunajivunia kuwa naye na tuna deni kutokana na uhusiano wetu mkubwa,” Rais Uhuru alisema. Alimweleza Rais Kikwete kuwa, katika utawala wake, alisimamia ajenda ya kuimarisha Jumuiya ya Afrika Mashariki na biashara kati ya Kenya na Tanzania ambayo alisema imefikia nusu kwa nusu.
“Katika utawala wako pia umesimamia sana masuala ya miundombinu ya kuunganisha nchi zetu. Barabara ya Arusha – Athi uliyozindua na Rais mstaafu Mwai Kibaki na ile ya juzi ya Voi – Arusha ambayo itaunganisha na bandari ya Mombasa ni ushahidi tosha wa jinsi wa kuimarika kwa biashara kati ya nchi zetu,” alieleza.
Kuhusu gesi ya Mtwara, Rais Uhuru alisema mapinduzi hayo mapya katika maendeleo, pia yataisaidia Kenya kwani itapata nishati kwa bei rahisi na inayoaminika. “Maendeleo mapya katika mradi wa gesi ni eneo jingine ambalo Kenya itafaidika nalo, kwani tutanunua kwa bei rahisi na tutakuwa na nishati inayoaminika na hivyo kusaidia kujenga nchi yetu kiuchumi na kijamii.
“Asante sana kwa kazi nzuri,” alisema Rais Uhuru na kumtaja Rais Kikwete kama rafiki wa kweli na mwana Afrika Mashariki mahiri. Rais Kikwete anafahamika vizuri kwa Wakenya baada ya kusaidia kusuluhisha mgogoro wa kisiasa mwaka 2007 uliosababishwa na matokeo ya uchaguzi mkuu wa rais.
Aidha, Rais Uhuru alimweleza Rais Kikwete kuwa zipo changamoto zinazozikabili nchi zote mbili ambazo ni ugaidi, ujangili na matumizi ya dawa za kulevya ambazo alisema anaamini mrithi wa Kikwete ataendeleza mapambano dhidi ya changamoto hizo.
Kwa upande wake, Rais Kikwete alisema katika wiki chache zijazo, watasimamia masuala hayo ili yanayowezekana sasa yafanyike haraka ikiwamo kusaini makubaliano ya awali (MoU) kuhusu matumizi ya gesi kutoka mkoani Mtwara.
Rais Kikwete alikuwa Kenya kwa ziara ya siku tatu kwa mwaliko wa Rais Uhuru Kenyetta ambapo aliitumia nafasi hiyo kuwaaga Wakenya na Jumuiya ya Afrika Mashariki ambayo kwa sasa ni mwenyekiti wake.
Chanzo: Habari leo
0 comments