Sudan Kusini inajiandaa kucheza mechi yake ya kwanza kabisa ya kufuzu kwa Kombe la Dunia itakapokutana na Mauritania Jumatano.
Taifa hilo changa zaidi duniani lilijiunga na shirikisho la soka duniani 2012, mwaka mmoja baada ya uhuru kutoka kwa Sudan.
Hata hivyo, nchi hiyo itaenda kwa mechi hiyo ya kwanza ya awamu ya mwanzo ya kufuzu kwa Kombe la Dunia ikiwa na imani zaidi baada ya kushinda mechi yake ya kwanza kabisa ya ushindani kimataifa.
Timu ya taifa hilo ililaza Equatorial Guinea 1-0 Septemba 5 kwenye mechi ya kufuzu kwa Kombe la Taifa Bingwa Afrika.
"Tuko tayari, tayari kabisa. Tunajua tunahitaji kufanya nini na tunaweza tukawashangaza wapinzani wetu,” nahodha wa Sudan Kusini Richard Justin Lado aliambia tovuti ya Fifa.
"Kocha wetu Sung-Jea Lee ametufundisha mfumo wa uchezaji ambao unatilia maanani nidhamu katika kujilinda na kucheza mashambulizi ya kujibu. Ninaamini tunaweza kuumiza wapinzani wetu. Tunahitaji kushinda, kwa sababu nyingi, na tutashinda.”
Wapinzani wao Mauritania wameorodheshwa nafasi 55 juu ya Sudan Kusini kwa viwango vya ubora wa soka duniani.
Hii ina maana kwamba watajaribu sana kuwazima mechi ya kwanza na kumaliza kazi watakapokuwa wenyeji wa mechi ya marudiano Jumanne Oktoba 13.
0 comments