Saturday 24 October 2015

LOWASA AWAOMBEA KURA WABUNGE NA MADIWANA WA CCM

By    

MGOMBEA urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), anayeungwa mkono na mwavuli wa Ukawa, Edward Lowassa, amejikuta akiombea kura wabunge na madiwani waliosimamishwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Akizungumza katika kampeni zake Ifakara mkoani Morogoro jana, zinazotarajiwa kuhitimishwa leo jijini Dar es Salaam, Lowassa aliomba wananchi wampigie kura ya urais yeye, lakini madiwani na wabunge wapewe wa CCM.

Kutokana na kauli hiyo iliyotolewa mbele ya umati wa watu, huku mkutano huo ukirushwa moja kwa moja na moja ya televisheni kubwa hapa nchini, baadhi ya viongozi wa Ukawa walichukua kipaza sauti na kumpa muda wa kutafakari, kabla ya kuendelea kuomba kura.

Hali hiyo ambayo haikutarajiwa na wengi ambayo pia haikutolewa ufafanuzi, ni sehemu ya baadhi ya matukio yasiyotarajiwa ambayo yamekuwa yakimtokea mgombea huyo.

Mwishoni mwa wiki hii, alipokuwa katika mahojiano na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), Lowassa alipotakiwa kueleza namna atakavyopambana na ufisadi katika ngazi ya juu, kwa maana ya rushwa kubwa, alijikuta akisema ufisadi ni swali gumu.

Akifafanua zaidi Lowassa alisema swali hilo mbali na ugumu, lakini pia ni refu na lingetaka kuwa na mjadala wake peke yake, huku akisema katika rushwa ndogo, baada ya kutafakari ameona kwa kuanzia ni kuwa na kituo kimoja cha kutoa huduma zote za Serikali, ili kupunguza urasimu.

CHANZO: HABARI LEO

0 comments