Friday 23 October 2015

WAATHIRIKA WA MAFURIKO KILOSA KUSUSIA UCHAGUZI

By    

Kaya 200 zenye watu zaidi ya 1,500 waliothirika na mafuriko mwaka jana na kuishi katika mahema katika kijiji cha  mateteni, wilayani Kilosa, mkoa wa  Morogoro wameazimia kutoshiriki kupiga kura katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Jumapili hii.

Kaya hizo zimefikia uamuzi huo kwa kile walichoeleza kuwa, serikali imeshindwa kuwapa makazi ya kudumu hivyo kuendelea kuishi maisha magumu kwenye mahema yaliyochakaa na wengine kulazimika kulala nje kwa kukosa makazi.

Akizungumza kwa niaba ya wathirika wenzake,  Saston Bwile, alisema baada ya ya kukumbwa na mafuriko mwaka jana, serikali kupitia viongozi mbalimbali akiwamo Waziri Mkuu Mizengo Pinda na Rais Jakaya Kikwete walitoa ahadi mbalimbali za kuwasaidia lakini mpaka sasa hakuna iliyotekelezwa.

Alisema Rais Kikwete alipowatembelea katika eneo hilo aliiagiza serikali ya wilaya ya Kilosa kuwapa viwanja vya kujenga makazi mapya kutokana na nyumba zao kubomoka na nyingine kusombwa na maji lakini ahadi hiyo haijatekelezwa.

Naye Salma Rashidi ambaye pia ni muathirika wa mafuriko hayo anayeishi katika mahema, alisema wameamua kutoshiriki uchaguzi huo kutokana na kuendelea kuishi kwa mateso ikiwamo kuathiriwa na upepo mkali hasa watoto wao.

Alisema upepo makali hasa majira ya usiku umewaathiri watoto wachanga wanane ambao wameugua ugonjwa wa nimonia kutokana na kulala nje na mama zao.

Naye kiongozi wa kijiji cha Mateteni, Iddi Ally, alisema wananchi hao wameamua kugomea uchaguzi mkuu kutokana na serikali kushindwa kutimiza ahadi zake hivyo wamekata tamaa kutokana na maisha magumu wanayoishi.

Alisema kutokana na hali hiyo, baadhi ya waathirika wamelazimika kurudi katika makazi yao ya awali ingiwa si salama kutokana na kuchoshwa na maisha magumu katika kambi hiyo, huku baadhi wakiishi kwa kulima vibarua ili kupata fedha za kujikimu.

Alisema licha ya jitihada mbalimbali za wao kama viongozi kufuatilia ahadi hizo ikiwamo Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, mpaka sasa hakuna majibu ya kupata viwanja ingawa eneo hilo limezungukwa na mashamba pori makubwa ambayo hayajawahi kuendelezwa.

CHANZO: NIPASHE

0 comments