Thursday, 8 March 2018

TFDA YAPIGA MARUFUKU NYAMA KUTOKA 'KUSINI'

MAMLAKA ya Chakula na Dawa (TFDA) imepiga marufuku uingizaji wa bidhaa za nyama kutoka Afrika Kusini, kufuatia mlipuko wa ugonjwa uitwao Lesterisis katika nchi hiyo.

Ugonjwa huo umehusishwa na ulaji wa bidhaa za nyama, zenye uchafuzi wa bakterria aina ya Listeria Monocytogees. Tayari watu kadhaa wameugua na wengine 180 wamepoteza maisha nchini Afrika Kusini kutokana na ulaji wa bidhaa za nyama. Taarifa ya TFDA iliyosainiwa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu, Agness Kijo ilisema mamlaka hiyo imesitisha vibali vya uingizaji bidhaa za nyama kutoka Afrika Kusini.

“TFDA imesitisha utoaji wa bibali vya uigizaji nchini wa bidhaa nyama kutoka Afrika Kusini kuanzia leo Machi 7, hadi hapo itakapothibitishwa na mamlaka ya nchi hiyo kuwa bidhaa hizo ni salama,” alisema Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TFDA.

Aina ya bidhaa za nyama zilizohusishwa na mlipuko wa huo ni sausages na polany aina ya viennes, russians, frunkfurturs, ambazo husindikwa na kampuni za Enterprise Food Production na Rainbow Chicken Limited za Afrika Kusni. Alisema TFDA kupitia mifumo yake ya udhibiti chakula, inaendelea kufanya ukaguzi na ufuatiliaji wa kina, kubaini uwepo wa bidhaa hizo katika soko na kuzuia uuzwaji wake, ikiwa ni pamoja na kuchukua hatua zaidi kwa mujibu wa sheria. Taarifa hiyo ya TFDA ilitoa wito kwa yeyote, atakayebaini uwepo katika soko la Tanzania wa bidhaa tajwa kutoka Afrika Kusini, kuacha kuzitumia na kutoa taarifa.

CHANZO : Habari leo

0 comments