Thursday, 8 March 2018

ZANZIBAR KUTENGENEZA SIMU ZA MKONONI

ZANZIBAR inatarajia kujenga kiwanda cha kuunganisha na kutengeneza simu za mkononi na kutoa ajira kwa wananchi wa visiwa hivyo.

Kiwanda hicho kitakachoanzishwa hivi karibuni na Kampuni ya U$I kutoka Korea Kusini, kitaanza kwa kuunganisha vifaa vya simu na kisha baada ya miaka minne kuanza kutengeneza simu. Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Ayoub Mohamed Mahmoud alisema kwa sasa wanaanzisha viwanda vikubwa vyenye kukuza uzalishaji, kuleta ajira na kukuza pato la taifa.

Alisema wiki mbili zilizopita, wamesaini makubaliano na kiwanda cha simu za mkononi na tayari wawekezaji hao wamepewa eneo katika eneo la viwanda vidogo. “Kwa sasa wanamalizia taratibu na wamesema katika miezi miwili hadi mitatu watakuwa wameanza kazi ya kuunganisha simu kutoka Korea Kusini, badala ya kununua kutoka Korea sasa zitakamilika hapa na kwenda kuuzwa maeneo mengine,” alisema.

Alisema kiwanda hicho anachodhani hakuna katika nchi za Afrika Mashariki, kitaanza kwa kuajiri watu 60 hadi 120 kwa kuanzia. Lakini, alisema kwa mtazamo wa wawekezaji, kitaanza uzalishaji wa simu kamili baada ya miaka minne. Alisema kabla ya muda huo, watatoa fursa kwa vijana 10 kutoka Zanzibar kupata mafunzo ya ziada katika maeneo ya uzalishaji simu na kupata shahada za uzamili na uzamivu kwenye teknolojia hiyo, hivyo kuzalisha simu kutoka mkoa huo.

Alisema kwa sasa kuna viwanda vya uzalishaji maji, viwanda vidogo vya nguo, usindikaji wa lami Fumba na kuna kiwanda kinaanza Nyamanzi, kujenga nyumba. Kiwanda hicho kina uwezo wa kujenga nyumba ya kawaida kwa siku tisa.

Alisema katika uchumi wa viwanda, Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein ameagiza kuwa katika kila mkoa, kila wilaya iwe na kiwanda cha mkakati angalau kimoja na sasa wanabainisha maeneo. Kwamba katika mkoa wake, kwa sasa wanaangalia aina ya viwanda vya kuanzisha na upatikanaji wa rasilimali, kwani maeneo mengi yametumika kwa makazi na yaliyobaki yanatumika kwa kilimo cha mazao ya viungo mbalimbali.

Chanzo : Habari leo

0 comments