Tuesday, 22 October 2013

WAFUASI WA PONDA WAPATA AHUENI

MAHAKAM A Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imetengua adhabu ya kifungo cha mwaka mmoja jela iliyotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam Machi 21 mwaka huu, dhidi ya wafuasi 52 wa Sheikh Ponda Issa Ponda, kwa sababu ilitolewa kinyume cha sheria husika.

Hukumu ya rufaa hiyo ilitolewa jana asubuhi na Jaji Salvatory Bongole, akisema kuwa Agosti 12 mwaka huu, alisikiliza hoja za wakili wa waomba rufaa (Mohamed Tibanyendera) na hoja zilizotolewa na mawakili wa serikali Peter Njike.

Katika maombi hayo, wakili Tibanyendera alichambua kosa la kula njama kutenda kosa kinyume cha kifungu 384 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2002.

Pia alichambua kosa la pili la kufanya mkusanyiko haramu kinyume na kifungu cha 74 na 75 cha sheria hiyo ambavyo vinasomwa pamoja na kifungu cha 43(2)(4) na 46 cha Sheria ya Jeshi la Polisi ya mwaka 2002.

“Kwa masikitiko makubwa tunasema kosa la kula njama halikuthibitika na Hakimu Fimbo alikosea kuwatia hatiani kwa kosa la kula njama kwa kutumia kifungu hicho cha 384 cha sheria ya Kanuni ya adhabu.

“Na kwa mujibu wa kifungu cha 46 cha Sheria ya Jeshi la Polisi ya mwaka 2002, mtu anayekutwa na hatia ya kutenda kosa la mkusanyiko haramu atapaswa alipe faini ya sh 50,000 au kwenda jela miezi mitatu au vyote pamoja,” alisema.

Wakili Tibanyendera alisema anashangaa Hakimu Fimbo kutoa adhabu ya juu kabisa ya mwaka mmoja jela, na hivyo kuiomba mahakama itengue hukumu hiyo kwani ina dosari nyingi za kisheria na kutokuwapo na ushahidi wowote wa kuweza kuishawishi mahakama hiyo iwatie hatiani waomba rufaa.

Naye wakili wa serikali, Njike aliiomba mahakama isitengue hukumu hiyo kwa sababu ilikuwa sahihi kisheria na kwamba upande wa jamhuri ulileta ushahidi mzito ambao uliishawishi mahakama ya Kisutu kuwatia hatiani washtakiwa hao kwa makosa matatu ya kula njama, kufanya maandamano haramu na kukaidi amri ya polisi.

Akitoa hukumu ya rufaa hiyo jana, Jaji Bongole alisema anakubaliana na wakili wa waomba rufaa kuwa Hakimu Fimbo alikosea kuwatia hatiani katika kosa la kwanza la kula njama.

Aidha Jaji Bongole alisema hakubaliani na ombi la waomba rufaa lililotaka mahakama iwaachilie katika kosa la pili la kufanya maandamano haramu kwenda katika ofisi za Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).

Wafuasi hao walikwenda kushinikiza amwachilie huru Ponda aliyekuwa akikabiliwa na kesi ya wizi wa malighafi na uchochezi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, ambayo ilimhukumu kifungo cha nje cha mwaka mmoja.

“Mahakama hii imekataa kuwaachilia huru katika kosa la pili la kufanya maandamano haramu kwenda ofisi ya DPP na pia imekataa kuwaachilia huru katika kosa la tatu na kukaidi amri ya jeshi la polisi iliyowataka watawanyike.

“Upande wa jamhuri uliweza kuleta ushahidi ambao umethibitisha waomba rufaa walitenda makosa hayo mawili na kwamba Mahakama Kuu inawatia hatiani kwa makosa hayo kwani mahakama ya Kisutu ilikuwa sahihi kuwatia hatiani,” alisema.

Jaji Bongole alisema pamoja na mahakama yake kuwatia hatiani katika makosa hayo mawili ambapo kwa mujibu wa sheria ya polisi, mtu anayepatikana na hatia katika makosa hayo anapewe adhabu ya kutumikia kifungo cha miezi mitatu jela na faini ya sh 50,000, mahakama yake inawapatia adhabu.

Kwamba hakimu wa Mahakama ya Kisutu alikosea kuwapatia adhabu ya kifungo cha mwaka mmoja.

Alisema licha ya mahakama kuwapatia adhabu hiyo, pia mahakama yake imeona washtakiwa ambao walikuwa wakitumikia adhabu ya mwaka mmoja gerezani tayari wameishakaa muda mrefu na adhabu ya kisheria kwa mujibu wa makosa hayo ya miezi mitatu imeishapita.

“Hivyo mahakama yangu inawaachilia huru ila kama waomba rufaa hao wana kesi nyingine, waendelee kushikiliwa na mamlaka nyingine,” alisema.

Hata hivyo gazeti hili saa nne asubuhi lilishuhudia waomba rufaa hao wakipakizwa kwenye basi la magereza na kurudishwa gerezani hadi pale mahakama itakapopelekewa hati inayoonyesha kwamba wameachiwa na mahakama hiyo.

Kesi hiyo, ilifunguliwa rasmi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Februari 18 mwaka huu, mbele ya Hakimu Mkazi, Sundi Fimbo, na siku hiyo hiyo upande wa jamhuri ukasema upelelezi umekamilika.

Machi 21 mwaka huu, mahakama hiyo ilimaliza kusikiliza kesi hiyo kwa kutoa hukumu ya kuwafunga jela mwaka mmoja kwa makosa hayo.



chanzo: TANZANA DAIMA

0 comments