WAZIRI
wa maji, Prof Jumanne Maghembe ameelezea kukerwa kwake na shirika la
umeme nchini (TANESCO) kwa madai limeshindwa kufikisha umeme vijijini na
hivyo miradi ya maji kusuasua.
Kadhalika waziri huyo ametamani kuwapo kwa shirika mbadala
ambalo litatoa ushindani kwa TANESCO ili iweze kutekeleza shughuli zake
na hivyo miradi ya maji kukamilika kwa watati.
“Tungekuwa na mashirika mengine ya umeme tungeweza kufungiwa umeme haraka, lakini kwa vile ni TANESCO peke
yake, sasa wananchi hawana maji…. TANESCO, ukiritimba too much,” alisema.
Profesa Maghembe alisema hayo wakati anazindua mradi wa
usambazaji majisafi katika kata ya Kiboroloni na viunga vyake, kwani
maeneo hayo yalikosa huduma hiyo muda mrefu, huku mipango ya kusambaza
katika kata za Ng'ambo na Msaranga ikiendelea.
Alisema wizara yake inatambua kuwa vijiji 74 katika mkoa wa Kilimanjaro
havina maji lakini mipango ni kuhakikisha hadi kufikia mwisho wa mwaka
huu vinapata huduma hiyo.
Aidha waziri huyo alisema kati ya vijiji hivyo 74, ni vijiji 28 ambavyo
miradi yake imekamilika na wananchi wanapata huduma hiyo huku Vijiji 17
miradi yake ipo katika hatua za mwisho lakini tatizo lililopo ni
kukosekana kwa umeme.
“Lakini kwa kweli tatizo tulilonalo sasa ni Tanesco…. Kwa muundo walionao ni lazima TANESCO wapandishe soksi zao juu,” alisema.
Alisema hata hivyo vijiji vingine 26 vipo katika hatua mbalimbali
za utekelezaji wa miradi ya upatikanaji maji na kwamba katika bajeti
ya mwaka huu,mipango ni kuvipatia maji vijiji 25 kila wilaya nchini.
Alimtaka mkurugenzi wa mamlaka ya majisafi na majitaka mjini Moshi
(MUWSA),Cyprian Luhemeja kuhakikisha hadi kufikia Juni mwaka
huu wananchi wote wa Moshi wapate maji.
Naye mkurugenzi wa MUWSA, mhandisi Luhemeja alisema mamlaka
imejiwekea vipaumbele Vya kupunguza upotevu wa maji kutoka Asilimia 38
Juni mwaka jana ingawa ilipofika Desemba mwaka jana kiango kilishuka
hadi asilimia 24 lengo likiwa kufikia asilimia 9 Desemba mwaka huu.
Vipaumbele vingine ni kuongeza kutoka idadi ya sasa zaidi ya 20,000 hadi
35,000, wamefanikiwa kuongeza chanzo cha coffee curing chenye lita za
ujazo wa 1500 huku juhudi za kuchimba kisima katika tanki la Kilimanjaro
kitakachokuwa na lita za ujazo 1800 kwa siku zikiendelea.
Alisema mamlaka ilijipa siku 180 kutekeleza mipango yake
ambapo walikusudia kukarabati miundombinu na kuondoa mtandao mbovu
wenye urefu wa Km 85 lakini hadi kufikia juzi mchakato wa kuondoa Km
24 umekamilika ambapo vifaa vimeshanunuliwa.
via Lukwangule blog
0 comments