Wednesday 15 July 2015

POLISI LA MSAFISHA MUHINDI ALIYEKAMATWA NA mil 772 DODOMA

By    
JESHI la Polisi mkoani Dodoma limesema Raia wa India, Amit Kevalramani (31) mfanyabiashara, mkazi wa Dar es Salaam aliyekamatwa na Sh milioni 772 katika Hoteli ya St Gasper Mjini Dodoma wiki iliyopita hana hatia yoyote, kwani hakuna tuhuma zozote za rushwa zilizothibitika.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, David Misime alisema hakuna tuhuma zozote za rushwa zinazomhusisha moja kwa moja na masuala ya uchaguzi.

“Katika tukio hili na uchunguzi tulioufanya, tumebaini kuwa hakuna kosa la jinai lililothibitika licha ya kukutwa na kiasi hicho cha fedha, tuhuma za rushwa ambazo ndiyo zilikuwa msingi wa ukamataji wa mtu huyo hazikuthibitika, kwani hakuna aliyeona akizigawa fedha hizo wala hakuna aliyedai kushawishiwa au kugawiwa fedha hizo,” alisema.

Akielezea mazingira ya tukio hilo, Misime alisema Julai 11, mwaka huu katika Hoteli ya St. Gasper ya mjini Dodoma, wananchi walitoa taarifa majira ya saa 10:00 jioni kuwa kuna mtu mmoja mwenye asili ya Kiasia, amekamatwa na wananchi akiwa na fedha nyingi na kuna vurugu kubwa.

Alisema baada ya kupata taarifa hizo, polisi walifika eneo la tukio ili kuona kama taarifa hizo ni za kweli.

“Askari walithibitisha kuwa ni kweli walimkuta mtu mmoja mwenye asili ya Kiasia akiwa na fedha kiasi cha milioni 722.5 na alipohojiwa alisema alifika Dodoma kwa ajili ya ununuzi wa mazao ya nafaka,” alisema.

Misime alisema kwa mujibu wa mtu huyo, alifika Dodoma Julai 10, mwaka huu majira ya asubuhi na kufikia Hoteli ya St. Gasper na siku iliyofuata Julai 11, aliamua kurudisha fedha benki kutokana na kuona mkusanyiko wa watu wengi wasioeleweka na wenye viashiria vya vurugu.

Misime alisema mtu huyo akiwa katika harakati ya kurejesha fedha hizo benki, ndipo kundi la watu waliokuwa katika eneo la Hoteli ya St. Gasper, walimtilia shaka na kumzuia asiondoke na ndipo taarifa zilitolewa Polisi.

“Mashaka ya watu hao yalitokana na vuguvugu za kisiasa na mchakato wa uchaguzi kati ya makundi mbalimbali kuwa kuna watu wanahonga wajumbe,” alisema.

Alisema taarifa za aina hiyo, hata Jeshi la Polisi lilikuwa limepokea bila uthibitisho. Alisema Jeshi la Polisi limethibitisha kuwa fedha hizo ni mali yake halali na kwa kuwa hakuna ushahidi mwingine uliothibitisha vinginevyo, amerejeshewa fedha zake.

CHANZO: habari leo

0 comments