Tuesday, 18 February 2014

BARAZA LA MAIMAMU WA KENYA LAITAKA SERIKALI KUCHUNGUZA WAHUBIRI WANAOTOA MAFUNZO YA KIGAIDI

https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEjc_sXugDtiavEqLJuwKqTH2NDEIqFzg4ZJXVbvJzLXlHkhMAAUKxyBV-MPMsJMlEatsytw70kkJf62FlIj8W_HORHfsAl1NXR0UosoI8-_Xmr_RdkzT30Z24zqyLo4udwbrxeqgy_HJwvQ/s1600/imamu+kenya.jpg
Viongozi wa Baraza la Maimamu  wa Kenya (CIPK), wamehimiza serikali kuchunguza baadhi wahubiri wanaotoa mafunzo yanayodhamiriwa kuwasukumiza vijana wa Kiislamu katika ugaidi.

Mwenyekiti wa CIPK, Sheikh Mohammed Idriss alisema baraza hilo linapinga mafunzo yoyote ambayo yanalenga kuwaingiza vijana katika ugaidi, akiongeza kuwa wanaofanya hivyo wanalenga kujinufaisha binafsi.

“Polisi wanapaswa kuwakamata wale wanaoeneza mahubiri yanayowashinikiza vijana kujiingiza katika ugaidi na kuwachukulia hatua kali za kisheria,” alisema Sheikh Idriss.

Mwito huo wa CIPK umekuja wiki chache baada ya polisi kuvamia Msikiti Mussa mjini Mombasa kufuatia habari za kijasusi kuwa vijana walikuwa wakipewa mafunzo yenye msimamo mkali wa kidini. 

Kwenye msako huo, polisi walipata laptop, vitabu, kanda za video kati ya bidhaa zingine zenye jumbe za uchochezi na chuki.

0 comments