1. Beti ninazicharaza , swali langu lisomeke,
kwa hili nalonikwaza, majibu kwangu yafike,
sikunyingi nikiwaza, leo bora nifunguke,
Bibo kosa lake lipi, sokoni haliuziki?
2. Japo Bibo ni la kwanza, Korosho ni mbegu yake,
Korosho mnaziuza, Bibo mwalipiga teke,
nabaki najiuliza, vipi lisithaminike?
Bibo doa lake lipi, sokoni haliuziki?
3.Kuna vilivyosokoni, sioni ubora wake,
tena si vya ushindani, Bibo ni zaidi yake,
vinauzwa kwa thamani, ni za vipi swifa zake?
Bibo kasoroye ipi, sokoni haliuziki?
4. Mfano kwa Doriani, kero kubwa rihi yake,
tajihisi kinyaani, ni mbaya harufu yake,
halishikiki sakoni, ni ghali mauzo yake,
Bibo ubayake upi, sokoni haliuziki?
5. Na Fenesi mathalani, namna ya kula kwake,
maurimbo vidoleni, huo ndo ubaya wake,
linashika namba wani, sokoni tnafasi yake,
Bibo kosa lake lipi, sokoni haliuziki?
6. Mkasa mwingine tena, wa Bungo bahati yake,
ni mbegu zilizonona, ukakasi ladha yake,
mnofu wala halina, ni upi ubora wake?
Bibo doa lake lipi, sokoni haliuziki?
7. Beti ya mwisho kabisa, ni ya nane nambari yake,
nitamaliza mkasa, wa Bibo dhuluma kwake,
Bibo tunda bora hasa, zipo hapo swifa zake,
Bibo kosa lake lipi, sokoni haliuziki?
8. Bibo zuri limenona, hakuna mfano wake,
rangi yake imefana, ni utamu radha yake,
linanukia mwanana, lapendeza umbo lake,
Bibo doa lake lipi, sokoni haliuziki?
Omari Lusonzo (Mapambano)
Kipo Mashariki - Rufiji
Pwani - Tanzania.
0 comments