Rais Paul
Kagame wa Rwanda ameonya kwamba yeyote atakayewasaliti Wanyarwanda na
Serikali yake anastahili kuchukuliwa hatua kali na kwamba amejitolea
maisha yake kuijenga na kuhakikisha Rwanda inakuwa salama dhidi ya wote
wasio na mapenzi mema.Akizungumza katika ibada maalumu ya kuliombea
taifa juzi, Kagame aliwataka Wanyarwanda wote kuungana katika kusimamia
misingi sahihi na msimamo wao kama taifa, bila kujali tetesi zinazotoka
katika mataifa ya nje kuhusu wale waliotangaza kuisaliti Serikali yake.
Japokuwa
hakutaja moja kwa moja kuhusu tuhuma zinazoikabili Serikali yake
kuhusiana na mauaji ya aliyewahi kuwa Mkuu wake wa Ujasusi aliyeuawa
Januari mosi akiwa hotelini huko Afrika Kusini, Patrick Karegeya,
alisema wale wote wanaoigeuka nchi yao na kuchagua kuua raia wasio na
hatia kwa sababu zao binafsi wanastahili kushughulikiwa ipasavyo.
"Sitakuwa
na huruma na watu ambao wanasahau namna Rwanda ilivyowatengeneza na
kuwa hapo walipo na hatimaye wanaamua kuisaliti kwa kuua raia wa Rwanda
wasio na hatia, wakiwemo kinamama na watoto," aliongeza.
Alisema
Rwanda haina sababu ya kuhusishwa au kuwajibishwa kwa ajili ya wale
walioamua kuchukua njia zaidi na kufanya mambo yao kwa nia ya kuharibu
yale yaliyofanyika kwa ajili ya kuliimarisha taifa la Rwanda.
Aliwataka
viongozi wa Rwanda kutokusumbuliwa kwa yanayowakuta 'maadui wa taifa'
kwa kuwa Mungu aliwapa nguvu ya kujenga na pia kukilinda kile
walichokijenga, hivyo wale wanaosahau kwamba wana dhamana kwa
Wanyarwanda na kuamua kutenda mambo mabaya dhidi ya taifa lao ni hakika
kwamba wamesahau kuwa hawataweza kuwa juu ya watu wao.
"Mliponiapisha kuwa kiongozi wenu mliniagiza kwamba wakati wote niilinde nchi hii, kwa maana ya kusimama kwa ajili ya watu wake.
Lakini
kila mmoja miongoni mwenu ana wajibu, aidha kwa njia ya kuhubiri au
kukanusha tuhuma zozote za uongo kuhusu Rwanda," alisema Kagame kama
alivyokaririwa na gazeti la New Times la Rwanda.
Alisema
watu wa mataifa ya nje ambao wamekuwa wakiinyooshea kidole Kigali
wamekuwa wakifanya hivyo mara 1000 zaidi kwa ajili ya kulinda nchi zao.
Hakusita
kukumbusha kwamba wapo baadhi ya watu ambao wamekuwa wakitishia wazi
hadharani kutaka kuipindua Serikali na wamekuwa wakishiriki katika
mikakati ya ulipuaji wa mabomu yaliyosababisha mauaji ya raia kwenye Mji
wa Kigali.
Tutapambana
Mtandao
wa Chimreports.com uliripoti kwamba Kagame alionekana 'mwenye hasira'
aliposema: "Kwa wale waliotengenezwa na kuwa juu na Rwanda kisha
kutugeuka kama taifa tutapambana nao. Yeyote anayeidharau Rwanda
atashughulikiwa ipasavyo popote alipo."
Serikali ya Afrika Kusini
Msemaji
wa Wiara ya Mambo ya Nje ya Afrika Kusini, Clayson Monyela alisema
hajapata taarifa zozote kuhusu kauli hizo za Kagame na hata hivyo hawezi
kusungumzia suala hilo kwa kuwa liko nje ua uhusiano wa kidiplomasia
baina ya Rwanda na nchi yake.
Hiyo ni
kwa sababu Kagame hakutaja nchi yoyote katika hotuba yake hiyo ya
jumapili na Afrika Kusini haiwezi kuchukua hatua ya kujihisi kwamba
labda ndiyo inayohusika.
"Tukio
lililotokea Johannesburg liko chini ya uchunguzi wa polisi na wote
tunasubiri matokeo ya uchunguzi huo. Hatuna sababu ya kuanza kumhisi
mkuu yeyote wa nchi, hatuendeshi diplomasia yetu kwa mtindo huo,"
alisistiza.
Kejeli
Jumamosi
iliyopita, Waziri wa Ulinzi wa Rwanda, Jenerali James Kabarebe
alikaririwa na mtandao wa AFP akizungumzia yaliyomkuta Karegeya
aliyeuawa huko Afrika Kusini akisema: Unapochagua kuishi kama mbwa,
utakufa kama mbwa."
Alikaririwa
akisema, "Msipoteze muda wenu kwenye ripoti kwamba fulani aliuawa kwa
kutumia kamba katika gorofa ya saba kwenye nchi fulani. Unapochagua kuwa
mbwa, utakufa kama mbwa, na wafanya usafi watasafisha na kutupa kwenye
pipa la taka ili usiwachafue.
"Kimsingi
hayo ni mambo yanayowapata waliochagua kupitia njia hiyo. Hatuna la
kufanya juu yao, na hatuwezi kulaumiwa kwa ajili ya yanayowakuta,"
alisema.
Mauaji ya Karegeya
Mwili wa
Patrick Karegeya aliyekuwa mshirika wa Rais Kagame kisha kutofautiana na
kukimbilia uhamishoni nchini Afrika Kusini ulikutwa ukiwa kwenye chumba
cha hoteli mjini Johannesburg huku kukiwa na kitambaa chenye damu na
kamba kando yake.
Baada ya
polisi kueleza kwamba Karegeya aliuawa kwa kunyongwa, wasaidizi wake
waliituhumu Serikali ya Rwanda kwa kuhusika na mauaji hayo.
Karegeya
alikuwa mkuu wa usalama wa taifa akihusika na usalama wa nje wa Serikali
ya Rais Kagame. Mwaka 2004 alishushwa cheo kisha kukamatwa na kuswekwa
jela kwa miezi 18 kwa madai ya kwenda kinyume na mkuu wake wa kazi.
Alikimbia nchini Rwanda mwaka 2007.
Pamoja na
wapinzani wa Kagame kumtuhumu moja kwa moja kuhusika na mauaji hayo,
Serikali yake haikuwahi kukubali au kukanisha moja kwa moja, lakini kwa
kauli yake alisema juzi kwamba 'Hahitaji kuomba ruhusua kwa yeyote
anaposimamia ulinzi wa taifa lake."
0 comments