Friday, 7 March 2014

YASIYOFAA KABLA YA NDOA

Kila sifa njema zinamstahikia Allah Mola wa viumbe vyote. Swala na salamu zimuendee Mtume wetu Muhammad (swalla Allahu alaihi wa sallam) na ahli zake na maswahaba wake.
Ndugu zangu katika imaan, Allah (subuhanahu wata’ala) baada ya kutuumba wanaadamu na kutuainishia namna ya kuendeleza kizazi chetu, ili kututofautisha na viumbe vyengine kama vile wanyama sisi akatuwekea taratibu nzuri ya ndoa.

Ndoa ni sunnah katika sunnah za mitume na ni jambo lililopendekezw
a sana na Mtume wetu Muhammad (swalla Allahu alaihi wa sallam), kwani kutoka kwa Abdullah Ibn Masoud (radhi za Allah ziwe juu yake) amesema: “Tulikuwa pamoja na Mtume (swalla Allahu alaihi wa sallam) vijana tusio na kitu, Mtume akatuambia: “Enyi kusanyiko la vijana! Yeyote miongoni mwenu awezaye gharama za ndoa, basi na aoe. Kwani huko kuoa kunalifumba mno jicho na kuihifadhi sana tupu. Na asiye weza, basi na ajilazimishe swaumu, kwani huko (kufunga) ni kinga kwake (dhidi) ya machafu.” Imepokewa na Bukhary na Muslim.

Kinachosikitisha, leo hii Waislamu tumelipokea vizuri jambo hili ila katika utekelezaji wake tumekuwa tukiengeza na kufanya mambo ambayo yanakwenda kinyume na Uislamu na kupoteza lengo na makusudio mazima ya ndoa. Katika makala hii in sha Allah tutayataja baadhi ya mambo yanayo kwenda kinyume na Uislamu na ambayo yamezoeleka kufanywa katika jamii zetu ima na wazazi au wanandoa wenyewe kabala ya kufunga ndoa.

Kuwapa uhuru wa kuwa pamoja wachumba

Tunashuhudia kwa baadhi ya wazazi kuwa watoto wao wanapoposwa hutoa mwanya na uhuru wa kufanya watakacho watoto hao. Baada ya kupata fursa hii watoto hao huanza kukaa pamoja katika mabustani, kumbi za starehe na hata kufikia mtoto wa kike kwenda kulala kwa mchumba wake pasi na wazazi kusema chochote. Kufanya hivi ni kunyume na sheria ya Uislamu kwani wachumba bado ni mtu na asiyekuwa maharimu wake, hivyo yale yote yasiyofaa mtu kufanya kwa wasiokuwa maharimu wake yanatakiwa kuchungwa. Kama vile katazo la kukaa faragha kwa kauli ya Mtume (swalla Allahu alaihi wa salam) : “Hakai mwanamme na mwanamke peke yao (faragha) ila watatu wao ni Shaytwaan.” Imepokewa na At-Tirmidhiy.

Kuvishana pete

Baada ya kuchanganyika na watu wa dini nyegine kama vile wakiristo, tumeanza kushuhudia kuwa baadhi ya vijana wa kiislamu wanapotaka kufunga ndoa huanza kwa kuvishana pete. Hakika jambo hili si katika Uislamu na ni juu yetu kujitahadhari nalo pamoja na mila nyengine za mayahudi na wakiristo kama anavyotutanabahisha Allah (subuhanahu wata’ala) : “Mayahudi hawawi radhi nawe, wala Wakristo, mpaka ufuate mila yao ...” [Al-Baqara (2) : 120]

Kitchen Party na yenye kufanana nayo

Imekuwa moja katika masharti ya harusi siku hizi ni kitchen party, na kama itakosekanwa basi harusi huwa haisihi kwa mtazamo wa baadhi ya dada zetu na mama zetu. Kitchen party hufanywa kwa lengo la kumchangia bibi harusi vyombo vya jikoni. Lakini jee, kumchangia huku hakuwezekani mpaka kukodiwe maholi na masteji? Jee wakati wa Mtume (swalla Allahu alaihi wa sallam) lilikuwepo hili? Mbali na ubaya wake wa kumtoa bibi haruhu mtupu katika steji jambo ambalo ni kinyume na Uislamu pia ni mila katika mila za kikafiri, hivyo ni wajibu wetu kujiepusha nalo.

Uradi au maulidi

Kwa kuonekanwa ubaya wa kitchen party na kukemewa na masheikhe jamii yetu ya wajanja ikaamua kuyasilimisha mambo hayo na kuleta uradi au wengine husoma maulidi. Kwa ghafla utaona ni jambo zuri hasa kwa jila lake-uradi- lakini jee ni dua tu zinazosoma katika huu uradi? Nimewasikia mwenyewe baadhi ya kina mama wakiulizia uhalali wa huu uradi maana mwisho wake hupigwa ngoma na marusha roho, pia huchanganyiaka maustadhi wa kiume pamoja na wanaweke katika usomaji wa uradi huo. Bila ya shaka hili si jambo lililofundishwa katika Uislamu.

Singo

Singo au kusingwa hufanywa kwa wote bibi harusi na bwana harusi. Kitendo hichi huhusisha kukogeshwa na kusafishwa kiwiliwili na kawaida hufanya na madada wa baba wadogo (watani). Baadhi ya wazee hasa wa kike hufikia kuwaambia watoto wao wa kiume huna radhi zangu kama utakataa kusingwa. Jee ruhusa hii ya kukaa wanawake na mwanamme pamoja imetoka wapi? Huku kukoshwa baleghe zima la kiume na dada zake ni Uislamu? Mtume (swalla Allahu alaihi wa sallam) amewataka wazee kuwatenganisha watoto wa kike na wa kiume katika malazi wafikapo miaka saba, leo iweje wakogeshane? Mtume (swalla Allahu alaihi wa sallam) amesema: “Ni bora mmoja wenu kugongelewa msumari katika utosi wa kichwa chake kuliko kugusa mkono wa mwanamke asiye halali yake” Iweje leo turuhusu kusuguana mtu na dada zake ambao si maharimu wake kwa kumkosha? Umefika wakati sasa wa jamii ya Kiislamu kuzinduka na kuacha mila ambazo zinakwenda kinyume na dini yetu tukufu.

Ndugu wa kiislamu, Uislamu tayari umeshakamilika kama Allah anavyolithibitisha hilo kwa kusema : “ ... Leo nimekukamiliishieni Dini yenu, na nimekutimizieni neema yangu, na nimekupendeleeni UISLAMU uwe ndiyo Dini ...” [Al-Maida (5) : 3]. Hivyo hatuna haja ya kufanya ambayo hayakufundisha na Uislamu, ima kwa kuwa ni mila za wazee wetu au ni mila za kikafiri zilizopendezeshwa katika macho yetu.

Kwa kumalizia, naiusia nafsi yangu na kuziusia nafsi zenu juu ya kufuata yale tuliyoamrishwa na kuacha yale tuliyokatazwa kama Mtume (swalla Allahu alaihi wa sallam) anavyotuambia: “Kile nilichokukatazeni kiepukeni, Na kile nilichokuamrisheni fanyeni kwa wingi kadiri muwezavyo. Hakika kilichowaangamiza watu wa Umma zilizopita, ni masuala (mahojiano) mengi na kupingana na Mitume yao.” Imepokewa na Bukhary na Muslim.

Allah atujaalie tuwe wenye kusika ya kheri na kuyafuata na kusika ya shari na kuyawacha. Amin.

0 comments