WANAFUNZI wa Kidato cha Nne, watafanya
mitihani miwili ya Taifa mwaka huu, baada ya kuongezwa mtihani wa
Matokeo Makubwa Sasa (BRN), ambao utatumika kuwapima walivyojiandaa na
Mtihani wa Taifa wa Kumaliza Elimu ya Sekondari.
Mkurugenzi wa Elimu ya Sekondari,
Paulina Mkonongo, alitangaza utaratibu huo jana na kufafanua kwamba
lengo ni kubaini wanaohitaji msaada kabla ya mtihani wa mwisho, ili
kuboresha taaluma darasani.
Kwa mujibu wa Paulina, mtihani huo wa
BRN, utafanyika kwa masomo machache lakini yanayosomwa na wanafunzi wote
ambayo ni Baiolojia, Hisabati, Kiswahili na Kiingereza.
Paulina alisema mtihani huo wa
majaribio, tayari umeanza kuandaliwa na utasambazwa kwa maofisa Elimu
nchini ifikapo Mei 10 mwaka huu, na barua kuhusu kufanyika kwa mtihani
huo imeshatumwa kwa makatibu tawala wote, ili kuanza maandalizi.
Matokeo ya mtihani huo, yanatarajiwa
kutumika kubaini mada ngumu kwa wanafunzi, wanaohitaji msaada na kuwapa
walimu mwanga kuhusu wapi wanafunzi hao wanahitaji msaada na lengo ni
kuongeza ufaulu kwa wanafunzi.
Tayari tangu mwaka jana mikoa 12 ilianza
kushiriki katika programu iliyohusisha mafunzo kwa walimu 4,064 wa
masomo husika, na mikoa 13 iliyosalia itashiriki programu hiyo mwaka
huu.
Mafunzo ya walimu wa mikoa hiyo 13 kwa
mujibu wa Paulina, yatafanyika Juni 2014 na programu ya mafunzo
rekebishi kwa wanafunzi wenye upungufu, itaanza Julai mwaka huu
kulingana na matokeo ya mtihani watakaofanya.
“Tutatoa mtihani wa majaribio kwa
wanafunzi wa kidato cha nne, ili kubaini maeneo yenye wanafunzi
wanaohitaji msaada zaidi na kutoa utaratibu wa mafunzo rekebishi na
mafunzo kazini, ili kuwajengea uwezo walimu wa kuwasaidia wanafunzi
walioko kwenye hatari ya kutofanya vema,” alisema Paulina.
Hata hivyo, Paulina alisema katika
utekelezaji utoaji wa mtihani huo, wanakabiliwa na changamoto ya
kuwapatia mafunzo wakuu wa shule zisizo za serikali, kuchapisha kitabu
cha mwongozo na ziara za wasimamizi wa elimu katika ngazi mbalimbali
kutoa ushauri.
Tayari walimu wakuu 3,001 wa shule za
Serikali wamepatiwa mafunzo na Taasisi ya Uongozi wa Elimu Bagamoyo
(ADEM) katika maeneo yaliyoainishwa, huku kitabu hicho cha mwongozo
kikiwekwa kwenye tovuti ya Wizara.
Paulina alisema mikakati endelevu
iliyopo, inalenga kuendeleza mafunzo ya walimu kazini, ili kuwajengea
uwezo kulingana na wakati na mahitaji ya mitaala.
Mbali na mafunzo hayo, pia wanalenga
kuwajengea walimu tabia ya kutunga mitihani bora ya kupima mchakato wa
ufundishaji, kubaini wanafunzi wanaohitaji kusaidiwa zaidi, kubaini mada
ngumu na kutoa mafunzo rekebishi kwa wanafunzi.
Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza la
Mitihani Tanzania (NECTA), Dk Charles Msonde, alisema vitabu rekebishi
vitaonesha wanafunzi waliofanya vizuri katika kila swali, waliojibu
vibaya na swali lilikuwa likitaka nini.
Vitabu hivyo vitasaidia walimu na
wanafunzi kubaini makosa mbalimbali yanayofanywa na watahiniwa wakati wa
kujibu maswali na kutumia mbinu bora za kujibu maswali.
“Mwisho wa vitabu hivyo, kuna mada
zilizofanywa vizuri na vibaya na jinsi ya kusaidia walimu wahakikishe
wanafunzi wanafaulu mada hizo,” alisema.
Vitabu hivyo kwa shule za msingi
vimetolewa vya masomo ya Kiswahili, Hisabati, Kiingereza, Sayansi na Maarifa ya Jamii kwa ajili ya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi mwaka
2012 na 2013. Kwa sekondari, vimetolewa kwa masomo ya Hisabati, Uraia,
Historia, Jiografia, Kiswahili, Kiingereza, Baiolojia, Kemia na Fizikia
kwa mwaka huo.
Dk Msonde alisema Baraza pia limepewa
jukumu la kupanga shule katika makundi ya ubora wa ufaulu, ili kuongeza
kiwango cha ufaulu katika shule za msingi na sekondari, na kuwajengea
walimu na wanafunzi hali ya ushindani na kujitambua kama shule imepanda
au imeshuka.
Makundi ya ufaulu yatapangwa kwa kutumia
rangi za kijani kwa shule zenye ufaulu wa juu, njano kwa zenye ufaulu
wa kati na nyekundu kwa shule zenye ufaulu wa chini kwa shule za msingi
na sekondari.
0 comments