IMERIPOTIWA kwenye vyombo vya habari, kuwa Maaskofu 32 wa Kanisa Katoliki wametaka Tume ya Jaji oseph Warioba iheshimiwe'.
Ni habari kubwa, na kuna habari pia za matamko ya Maaskofu wa makanisa
mengine yasiyo ya Kikatoliki kuhusiana na Katiba. Matamko yaliyotolewa
kwenye majira ya Pasaka.
Binafsi nimeupitia ulioolezwa kuwa ni ' Ujumbe wa Kichungaji wa Pasaka 2014 kwa Waumini na Watu wote wenye Mapenzi Mema'.
Nachangia hapa kama mtu mwenye mapenzi mema. Kwamba naungana na
Maaskofu wetu hawa 32 kwenye hoja yao ya msingi; kwamba Tume ya Warioba
iheshimiwe, hivyo basi, mawazo ya wananchi pia yaheshimiwe.
Nyongeza
hapa, ni kuwa hata mawazo ya wachache nayo yaheshimiwe, na kwamba
wapewe uhuru wa kujenga hoja zao na hata kuwashawishi walio wengi
wakubaliane na hoja zao. Hiyo ndiyo demokrasia.
Maaskofu wetu
wametumia hekima nyingi kwenye andiko lao. Hawakuweka misimamo yao juu
ya mfumo upi wa muungano au serikali wanaoutaka. Wameelezea tu
wanachokiona na kushauri na labda kuelekeza, maana, nao ni wachungaji.
Ni viongozi. Wamesisitiza umuhimu wa uwepo wa umoja wenye kupigiwa
mfano. Lakini, wameonyesha pia haja ya kuwepo kwa mabadiliko au mageuzi
ya kimsingi.
Naam, nchi yetu imetumia rasilimali fedha nyingi na
hata rasilimali wakati mwingi kwa kuipa, muda na fedha nyingi, Tume ya
Kuratibu Maoni ya Wananchi kuhusu Katiba chini ya Jaji Warioba.
Yumkini, si kila maoni yaliyotolewa yanampendeza kila mtu au kikundi cha
watu. Lakini, kwa vile tumekubaliana kutumia njia hiyo katika kufikia
maridhiano ya kupata Katiba mpya, basi, ni vema na ni busara tukawa
tayari kuyakubali na kuyaishi hata yale ambayo hatukuyapenda. Ni kwa
vile kuna wengine wengi wenye kuyataka.
Na wengine hao ni watu
wenye kustahili kusikilizwa matakwa yao. Na kimsingi, kama Taifa,
tunaweza kutumia mfumo wa Serikali moja, mbili au tatu, alimradi,
maamuzi hayo yajengwe katika misingi ya majadiliano na maridhiano. Bila
malengo ya kumpata mshindi na mshindwa. Hivyo basi, tukiondoa tofauti za
kiitikadi, tutabaki kuwa wamoja, na kitakachoamuliw a kitakuwa ni ushindi wetu wote kama taifa.
Tuking'ang'ania
kusimamia kwenye makundi yetu na vyama vyetu, na kimsingi tukitanguliza
maslahi binafsi, ya makundi na vyama, basi, hatari iliyo mbele yetu ni
kushindwa wote, kama alivyopata kutamka Rais Jakaya Kikwete.
Na
Rasimu hii ya Katiba, ukiacha hayo ya mifumo ya muungano na serikali,
ina mengi mengine yanayotokana na mawazo ya wananchi wenyewe.
Mchakato huu umekuwa ni zaidi ya kupata Katiba mpya, kwa Watanzania
wengi, umetoa fursa ya kupata ' elimu ya bure' juu ya somo la uraia.
Kwamba kupitia mchakato huu wengi wamepata uelewa wa mambo mengi kuhusu
nchi yao ambayo huko nyuma hawakuyajua. Si kuyapata tu, kwamba ni
Watanzania wenyewe waliochangia kwenye maarifa haya mapya.
Kwa
kuusoma waraka wa Maaskofu, na kwa kufuatilia mijadala hii ya sasa,
jambo moja ni dhahiri, wananchi wengi, wa Bara na Visiwani, wanataka
kuendelea na Muungano wao. Lakini, kuna waliyoyapendeke za ili kuimarisha Umoja na Ushirikiano wao. Maoni yao yasipuuzwe.
Na hakika, katika kipindi hiki tumeshuhudia kizungumkuti kwenye Bunge
Maalumu la Katiba. Na sasa tunamwona Mwenyekiti wa Bunge, Samuel Sitta
akifanya jitihada za makusudi kuhakikisha Bunge hili linaendelea, ni
katika kutafuta namna ya wenye kupingana wanafikia maridhiano ya namna
ya kwenda mbele.
Na hilo haswa ndilo jukumu la spika kama mwenyekiti
wa kikao cha bunge. Maana, hata ukisoma historia ya mabunge tangu karne
ya 17, na kwa kuiangalia Uingereza, unaona kuwa spika alikuwa na jukumu
kuu la kuwakilisha haki za wabunge dhidi ya korona (crown) ikiwa na
maana ya mamlaka ya kifalme. Na utaratibu huo umeendelea na imekuwa
sehemu ya tamaduni za kibunge.
Kwamba spika analiendesha bunge kwa
kufuata kanuni. Kwamba hana upande, kwa Waingereza, hata kama spika ni
mbunge, hapaswi kusimama na kulisemea jimbo lake la uchaguzi.
Wajibu
wa spika pia ni kulinda haki za makundi yote ndani ya bunge, na
hususan, haki za wachache. Spika akiwa mwanamume ni sawa na ' baba wa
wabunge' na akiwa mwanamke anakuwa ' mama wa wabunge'. Na mzazi hapaswi
kubagua wala kumpendelea waziwazi mtoto miongoni mwa watoto wake. Wote
ni wa kwake.
Tunapoliangalia
hili la Katiba yetu, kuna umuhimu wa kuwapo kwa ' mitazamo ya
kikatiba' kwa wajumbe wa Bunge la Katiba. Inahusu kinachoitwa '
constitutional thought'. Kwamba kukosekana kwa 'constitutional thought' kwenyewe kunaweza kuyumbisha Bunge la Katiba.
Kwamba fikra za wabunge zilipaswa ziwe za ' kikatiba zaidi', na hivyo
kutazama namna Katiba itakavyokuwa bila kujiangalia wao kwa sasa wamekaa
vipi, maana, watakachofikiri a
kitakuwa cha sasa zaidi, na pengine kesho inayoishia 2015, wakati
Katiba itakuwa ni ya kuishi kwa miaka ambayo hata wao na watoto wao
hawatakuwapo duniani.
CHANZO:RAIA MWEMA
CHANZO:RAIA MWEMA
0 comments