WIZARA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi,
imepigilia msumari kwa kuendelea kuwazuia wanafunzi wa shule za
sekondari za serikali za bweni na kutwa kumiliki simu za mkononi wakiwa
shuleni na yule atakayekamatwa hatua za kinidhamu zitachukuliwa dhidi
yake.
Licha ya kuendelea kukazia amri hiyo,
pia imetoa utaratibu unaowataka wakuu wa shule za sekondari za mabweni
kuzitumia ofisi za walimu wa malezi kuwa ni sehemu muafaka ya kuwasaidia
wanafunzi wenye matatizo mbalimbali ya kuwasiliana na wazazi na walezi
wao.
Kauli hiyo ilitolewa na Waziri wa Wizara
ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa, jana, wakati
alipojibu maswali ya wanafunzi wa Shule ya Sekondari Mzumbe, ambayo ni
ya wavulana wa vipaji maalumu, ambao baadhi yao walimwomba Waziri
aruhusu matumizi ya simu za mkononi kwa wanafunzi wa shule za sekondari
wakiwa shuleni.
Akijibu swali la msingi la Mwanafunzi
Hamis George wa kidato cha sita mchepuo wa PCB, ambaye alisema kuwa
hakuna mantiki yoyote kwa wakati huu Serikali kuendelea kupiga marufuku
kwa wanafunzi wa sekondari za serikali wa bweni kuwa na simu za mkononi
kwani zitawasaidia kuwasiliana na wazazi, walezi nyakati za shida
shuleni.
Hoja hiyo ilipingwa na Waziri Kawambwa
akisema kuwa maudhui ya uzuia simu za mkononi kwa wanafunzi wa shule za
sekondari za Serikali bado halijabadilika na litaendelea kuwepo kutokana
na hali halisi ya kimazingira yaliyopo.
“ Hili suala nikiwa Waziri mwenye
dhamana , siwezi kulitengua, litaendelea kusimama kama ilivyo, maelekezo
ni kwamba wakuu wa shule waandae utaratibu wa kuzitumia ofisi za walimu
wa malezi kuwa ni sehemu ya wanafunzi kupeleka matatizo yao yapatiwe
ufumbuzi na si kuruhusu mwanafunzi kuwa na simu shuleni,” alisema Waziri
huyo.
Hoja hiyo ya kuendelea kupinga marufuku
wanafunzi wa shule za sekondari kuwa na simu shuleni, iliungwa mkono na
Mkuu wa Wilaya ya Mvomero, Anthony Mtaka, ambaye aliwakata wanafunzi
kufuata kile kilichowaleta shuleni, kwani miaka minne ama miwili kwao si
mingi wakimaliza wataenda kukumbana na maisha ya kidunia mtaani.
“ Mwanafunzi upo hapa Mzumbe Sekondari
kwa ajili ya kusoma...kuwa na simu haikusaidii , kwanza utajipotezea
muda kwa kuchati na watu ama marafiki wa kike , mwishowe unafeli
mtihani, lawama zitaelekezwa serikalini…vuteni subira mambo haya
yanawasubiri baada ya kumaliza elimu yetu ya sekondari,” alisema Mkuu wa
Wilaya.
0 comments