Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana kuhusiana na utendaji wa shirika hilo katika kipindi cha serikali ya awamu ya nne, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo, Johnson Mfinanga, alisema katika kipindi hiki hicho Rais Kikwete aliliwezesha shirika hilo kuanzisha safari za kwenda visiwa vya Comoro na wamekuwa wakizidi kuongeza safari zaidi kuelekea huko kwa kuwa wamebaini uamuzi huo umekuwa na tija kwa wananchi wa mataifa hayo mawili.
“ATCL kwa sasa limeongeza idadi ya safari zake kuelekea visiwa hivyo kutoka mara tano hadi nane kwa wiki. Shirika hili ndilo pekee la ndege hapa nchini linalotoa huduma zake kutoka Dar es Salaam kuelekea visiwa vya Comoro na hivyo kutoa fursa kwa wananchi wake kuunganisha fursa mbalimbali zinazopatikana kwenye mataifa hayo ikiwamo biashara,” alisema.
Mfinanga alisema kwa sasa shirika hilo lina mpango wa kutambulisha safari zake za moja kwa moja kati ya visiwa vya Comoro na Zanzibar kabla ya mwisho wa mwaka huu kutokana na uhitaji mkubwa wa soko linachochewa na fursa za kibiashara baina ya visiwa hivyo.
Alisema shirika hilo pia linaendelea kuboresha huduma zake kuelekea mkoani Mtwara na linajivunia kuwa kiungo muhimu katika usafiri kutoka Dar es Salaam hadi katika mkoa huo ambao kwa sasa unajipanga kuchangamkia fursa ya uchumi wa gesi.
“Tumekuwa tukifanya safari zetu kuelekea mkoani Mtwara kwa kipindi kirefu sasa. Fursa ya gesi iliyoibuka mkoani humo inasababisha na sisi pia tujipange kwa kuangalia ni namna gani tutanufaika na fursa hiyo pia. Vile vile tuna jukumu la kuhakikisha tunatimiza wajibu wetu kama shirika la taifa katika kukabiliana na mahitaji ya wananchi wa taifa hili,’’ alisema.
Akizungumzia mipango ya shirika hilo katika kujipanua zaidi, Mfinanga alisema kwa sasa linaandaa mpango mkubwa wa miaka mitano ambao utawekwa wazi hivi karibuni.
CHANZO: NIPASHE
0 comments