TUME ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), imefuta kibali kilichoanzisha vyuo vikuu viwili vishiriki vya Chuo Kikuu cha Mtakatifu Joseph Tanzania (SJUIT).
Vyuo vilivyofutwa ni Chuo Kikuu Kishiriki cha Sayansi za Kilimo na Teknolojia (SJUCAST) na Chuo Kikuu Kishiriki cha Teknolojia ya Habari (SJUCIT) vilivyoko Songea mkoani Ruvuma.
Akizungumzia uamuzi huo Dar es Salaam jana, Katibu Mtendaji wa TCU, Profesa Yunus Mgaya, alisema hatua hiyo imetokana na vyuo hivyo kushindwa kutoa elimu ya chuo kikuu ya viwango stahiki.
Profesa Mgaya amesema vyuo hivyo vimekuwa na mlolongo wa matatizo ya ubora, uongozi na ukiukwaji wa sheria na taratibu za uendeshaji wa chuo kikuu, kama zilivyobainishwa na Sheria ya vyuo vikuu.
Alisema jitihada za Tume kutaka chuo hicho kuhakikisha kinatoa elimu inayokidhi viwango vya ubora, hazikupewa uzito stahiki na uongozi wa chuo na kusababisha wanafunzi kuendelea kuathirika.
Kutokana na hatua hiyo, Tume hiyo imeidhinisha uhamisho kwa wanafunzi wanaosoma katika vyuo hivyo kwa gharama za SJUIT, ikiwa ni pamoja na wanafunzi wa mwaka wa kwanza na wa pili wanaosoma shahada za kwanza.
Wanafunzi hao ni wanaochukua Shahada ya Kwanza ya Teknolojia ya Uhandisi wa Kilimo na Shahada ya Kwanza ya Teknolojia ya Uhandisi wa Usindikaji wa Chakula, ambao kwa sasa wanasoma katika Kampasi ya Luguruni, jijini Dar es Salaam.
Profesa Mgaya alisema wanafunzi 2,046 waliokuwa wakisoma katika vyuo hivyo watahamishiwa kwenye vyuo vikuu vingine vinavyofundisha programu za masomo zinazofanana na masomo wanayosoma hivi sasa.
Kwa mujibu wa Profesa Mgaya, wanafunzi wote wanapaswa kuondoka chuoni mara moja baada ya kukamilisha taratibu za kukabidhi mali na vifaa vingine vya chuo kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa.
Alitaka wanafunzi wote kuripoti kwenye vyuo watakavyopangiwa wakati wa kufunguliwa kwa muhula wa pili, kwa kufuata tarehe halisi ya kuanza kwa muhula huo kwa kila chuo watakachopangiwa. Tarehe hizo zitatangazwa kwenye tovuti ya TCU.
Kuhusu wanafunzi wanaosoma Shahada ya Kwanza ya Sayansi za Kilimo na Uhandisi, alisema watahamishiwa katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), wanaosoma Shahada ya Kwanza ya Ualimu wa Sayansi, watahamishiwa kati ya SUA, Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) na Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Mwenge (MWECAU).
Kwa mujibu wa Profesa Mgaya, orodha ya wanafunzi waliohamishwa na majina ya vyuo vikuu walivyohamishiwa, itatangazwa na kuwekwa kwenye tovuti ya vyuo vikuu husika.
Aidha, wanafunzi waliohamishwa ambao hawakukamilisha mitihani yao ya mwisho wa muhula wa kwanza au hawakufanya kabisa mitihani hiyo, watatakiwa kufanya mitihani hiyo katika vyuo vikuu watakavyohamishiwa kwa utaratibu maalumu utakaoandaliwa na chuo husika.
Alisema kila mwanafunzi anawajibika kutunza kumbukumbu zake zote muhimu za maendeleo ya kitaaluma kwa ajili ya matumizi ya baadaye, ikiwa ni pamoja na matokeo ya mitihani aliyokwishafanya.
Kwa wale ambao ni wanufaika wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), Profesa Mgaya alisema mikopo yao itahamishiwa katika vyuo watakapokuwa wamehamishiwa.
Chuo cha Mtakatifu Joseph ni mojawapo ya vyuo vikuu vilivyosajiliwa na TCU na kinamilikiwa na Shirika la Kitawa la Dada wa Maria Imakulata (DMI) pamoja na washirika wao. Chuo hicho kilianzishwa mwaka 2003 chini ya usajili wa Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) na mwaka 2013, TCU iliidhinisha maombi ya kuanzishwa kwa vyuo vikuu vishiriki.
Chanzo: Habari leo
0 comments