Wednesday, 17 February 2016

WANACHACHAMA WA CCM MKOANI MWANZA WAONYA VITEGA UCHUMI VYA CHAMA KUTUMIKA VIBAYA

By    
Wanachama wa Chama cha Mapinduzi CCM, Kata ya Kirumba Wilaya ya Ilemela Mkoani Mwanza, wameonya juu ya baadhi ya Wawekezaji nchini wanaotumia Vitega uchumi vya chama hicho bila kufuata mikataba wanayopewa.

Wanachama hao walitoa kauli hiyo wiki hii baada ya Wawekezaji wanaotumia majengo ya CCM Kata ya Kirumba, kudaiwa kukiuka masharti yao na hivyo kutumia majengo hayo bila kuyalipia kodi ya pango kwa muda mrefu.

Ni kutokana na hatua hiyo, Wanachama hao walichukua maamuzi ya kufunga Majengo hayo ambayo yanatumiwa na Tasisi ya Mikopo ya Wadoki pamoja na Hotel ya Kirumba Resort, huku taratibu nyingine za kisheria zikiendelea, lengo likiwa ni kuhakikisha kwamba watumiaji wa majengo hayo wanayalipia kodivwanayodaiwa vinginevyo watafurushwa nje ya majengo hayo.

Mwenyekiti wa CCM Kata ya Kirumba Abubakary Francis Kweyamba alithibitisha kwamba wanachama hao wamefikia maamuzi hayo, kutokana na kutumia majengo ya chama katika kata hiyo huku wakiwa hawayalipii kodi na hivyo kukisababishia chama usumbufu mkubwa wa kuendesha shughuli zake za kiofisi huku akisisitiza msimamo wa kuendelea kuyafunga majengo hayo.

Katibu Mwenezi wa CCM Kata ya Kirumba Juma Wesa pamoja na Katibu wa Chama hicho Wilaya ya Ilemela Acheni Maulidi, walisema kuwa maamuzi yaliyochukuliwa na wanachama hayo ni sahihi kwa kuwa malalamiko ya wawekezaji hao yaliishajadiliwa hadi ngazi ya Mkoa ya Chama hicho na kuonekana kwamba wawekezaji hao hawatii makubaliano yaliyofikiwa.

Suala hilo lilifikishwa katika Kituo cha Polisi Kirumba na kila upande umetakiwa kuwasilisha vielelezo vyake ili kutambua wanaokiuka makubaliano ya mkataba wa upangaji kwa ajili ya hatua zaidi za kisheria.

Meneja wa Kirumba Resort hakutaka kuzungumzia malalamiko hayo kwa madai kwamba mzungumzaji ni Mkurugenzi wake ambae alisema amesafiri huku Uongozi wa Wadoki Saccos ukishindwa kupatikana.
Imeandaliwa na George Binagi-GB Pazzo @BMG.


0 comments