Friday, 12 February 2016

WANAWAKE MWANZA WATAKIWA KUTOBWETEKA ILI KUACHANA NA UTEGEMEZI KATIKA JAMII.

By    
Kulia ni Bi.Vileth Muhamusi ambae ni mmoja wa Wajasiriamali Jijini Mwanza akizungumza na Mwandishi wa taarifa hii, George Binagi-GB Pazzo wa Binagi Media Group (BMG).

Wanawake Mkoani Mwanza wametakiwa kutobweteka na kukaa majumbani bila kujishughulisha na shughuli za uzalishaji mali, kwa kuwa hatua hiyo inawafanya kuwa tegemezi katika jamii.

Bi.Vileth Muhamusi ambae ni mmoja wa Wajasiriamali maarufu Jijini Mwanza, anaejishughulisha na biashara ya bustani hususani kuotesha miche mbalimbali ikiwemo miche ya mbao, matunda pamoja na kimvuli, aliyasema hayo jana wakati akizungumzia tatizo la ukosefu wa ajira kwa akina mama ambalo hivi sasa limegeuka janga kwa malezi ya watoto kutokana na baadhi yao kuwatumia watoto wao katika shughuli za kuomba omba mitaani ili kupata fedha za kujikimu kimaisha.

Bi.Muhamusi anaepatikana katika bustani zilizopo pembezoni mwa Ziwa Victoria katika barabara ya Makongoro Jijini Mwanza, alibainisha kwamba wanawake wanapaswa kuchukua hatua na kuachana na fikra za utegemezi, ikiwemo kujiunga na vikundi mbalimbali vya maendeleo, akitolea mfano kikundi chake kijulikanacho kama Mazingira Group, na kwamba kupitia vikundi hivyo wanawake wataweza kupiga hatua za kimaendeleo.

Alianza shughuli zake za kuotesha miche miaka mitano iliyopita, na ameweza kupata kipato cha kumuwezesha kujikimu kimaisha yeye pamoja na familia yake huku kubwa zaidi likiwa ni kumudu kuwasomesha watoto wake kutokana na biashara ya kuuza miche anayootesha, ambapo anabainisha kwamba biashara hiyo inalipa kwani kuna aina mbalimbali za miche ambayo ina soko kubwa, akitolea mfano miche ya Mitiki ambayo mche mmoja huuzwa hadi shilingi elfu tatu.

Hata hivyo bi.Muhanusi aliwatoa hofu wanawake juu ya suala la mitaji ambalo limekuwa likilalamikiwa na wengi, ambapo ametanabaisha kwamba shughuli nyingi za ujasiriamali ikiwemo ya bustani, hazigharimu mtaji mkubwa ikilinganisha na gharama za mahitaji yao ya kila siku kama vile gharama za saluni huku wakiwa hawana shughuli za kuwaingizia kipato.

Kauli ya Bi.Muhanusi iliungwa mkono na Edwin Soko ambae ni Mwenyekiti wa Chama cha Wajasiriamali Tanzania, aliebainisha kwamba ili wanawake waondokane na utegemezi ni vyema wakajitambua na kufungua fikra zao, kwani baadhi yao wamekuwa wakiwekeza katika matumizi mabaya ya fedha ikiwemo kutumia hadi shilingi elfu sabini kwa ajili ya urembo huku wakiwa hawana shughuli za uzalishaji mali, jambo ambalo linawakwamisha wengi wao kupiga hatua za kimaendeleo. 
Mmoja wa Vijana wanaootesha mbegu
Miche ya aina mbalimbali
Ukiona njiti za Viberiti, basi tambua kwamba zinatokana na miti hii ambayo inajulikana kwa jina la Mitiki. Miti ya Mitiki pia ni mizuri na imara kwa ajili ya mbao.
Picha na Hamza Makuza, BMG Mwanza.

0 comments