Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Masuala ya Wanawake, Wazee na Watoto wa Tanzania, Mh. Ummy Mwalimu akiwasilisha mada kuu ambapo aliwakilisha kundi la Afrika katika mkutano huo mkubwa unaoendelea nchini Marekani.
Bara la Afrika na hasa wanawake ndio wanaobeba mzigo zaidi wa madhara ya mabadiliko ya tabianchi, huku wakinyimwa fursa ya kushiriki katika kutafuta suluhu kwa tatizo hilo, ameeleza leo Ummy Mwalimu, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Masuala ya wanawake, wazee na watoto wa Tanzania.
Bi Mwalimu amesema hayo akihutubia kikao cha 60 cha Kamisheni ya Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya wanawake, CSW60 kwa niaba ya kundi la nchi za Afrika, akisisitiza umuhimu wa kushirikisha zaidi wanawake katika uongozi wa kimataifa kuhusu suala la mabadiliko ya tabianchi.
"Wanawake wanapaswa kuweza kuongoza katika ngazi za kitaifa na serikali za mitaa. Ubunifu wao, ujuzi wa kiasili, matarajio yao yanaweza kusaidia katika kubuni na kushawishi suluhu kuhusu mabadiliko ya tabianchi.”
Aidha amezungumzia suala la kilimo ambacho hushughulisha wanawake zaidi, akisema la msingi ni kusaidia sekta binafsi ili kukuza ukuaji wa uchumi katika sekta hiyo na hivyo kuwezesha wanawake.
Baadhi ya washiriki wa mkutano mkuu wa mwaka wa wanawake unaofanyika nchini Marekani ulioanza jana Machi 14-24, wakiwa nje ya jengo la Umoja wa Mataifa unapofanyika mkutano huo
Baadhi ya washiriki wakifuatilia mkutano huo wa #CSW60
0 comments