Sunday, 3 April 2016

MIZIGO YAPUNGUA BANDARI DAR

By    

WAKATI Mamlaka ya Bandari (TPA) ikithibitisha ufanisi katika upakuaji na uondoshaji mizigo na usalama wa mali katika Bandari ya Dar es Salaam, imebainika idadi ya mizigo katika bandari hiyo, imepungua tofauti na matarajio.

Akizungumza wakati akifunga warsha ya Wahariri wa Habari mwishoni mwa wiki, Kaimu Meneja wa Bandari ya Dar es Salaam, Hebel Mhanga, alitoa mfano wa shehena ya magari yanayokwenda Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC).

Kwa mujibu wa Mhanga, shehena ya magari yanayokwenda katika nchi hiyo kutoka Januari 2015 mpaka Januari 2016, imepungua kwa asilimia 50 huku shehena ya Zambia ikipungua kwa asilimia 46. Beira Mhanga alisema walipochunguza sababu ya kupungua kwa shehena hizo, walibaini sehemu ya shehena hiyo hasa iliyokuwa ikienda Zambia, DRC na Malawi, inashushwa katika Bandari ya Beira nchini Msumbiji.

Sababu za kushushwa katika Bandari ya Msumbiji, badala ya Bandari ya Dar es Salaam ambayo ndiyo yenye unafuu wa umbali kutokana na jiografia yake, Mhanga alisema ni unafuu wa kusafirisha shehena hiyo kwa reli ya Beira mpaka Malawi, tofauti na ilivyo kwa barabara.

Alisema usafirishaji wa reli ni nafuu kwa asilimia 30, ikilinganishwa na usafirishaji wa barabara na kwa kuwa Msumbiji wameshakamilisha ujenzi wa reli ya kisasa, wafanyabiashara wameona unafuu wa kupitisha mizigo katika Bandari ya Beira kuliko ya Dar es Salaam.

Athari hiyo katika Bandari ya Dar es Salaam, huenda ikawa mbaya zaidi baada ya kukamilika kwa reli ya kisasa inayoanzia katika Bandari ya Mombasa mpaka DRC, kwa kuwa itaongeza unafuu wa usafirishaji wa mizigo katika bandari hiyo shindani kwa Tanzania.

Katika warsha hiyo, ilifafanuliwa kuwa dunia nzima bandari zimekuwa na mafanikio, kutokana na kuwa na mfumo wa reli za kisasa unaotoa mizigo bandarini na kufikisha kwa mteja, jambo linalokosekana katika Bandari ya Dar es Salaam.

Taarifa zaidi tembelea http://www.habarileo.co.tz/index.php/habari-za-kitaifa/8130-mizigo-yapungua-bandari-ya-dar

0 comments