Friday, 24 June 2016

MAJALIWA AWATOA HOFU WATAHINIWA WA KIDATO CHA NNE

By    

WANAFUNZI wote waliofaulu Mtihani wa Taifa wa Kumaliza Kidato cha Nne, watapangiwa kwenda katika shule za Serikali na wengine watapangiwa kwenda vyuo kuchukua diploma.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alisema hayo bungeni jana katika kipindi cha maswali ya papo kwa hapo, alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Nsimbo, Richard Mbogo (CCM). Katika swali hilo, Mbogo alisema kuna taarifa zinazagaa kuwa mwaka huu serikali haitachukua wanafunzi waliofaulu kidato cha nne kwenda katika shule za kidato cha tano.

Akifafanua majibu yake, Majaliwa alisema taarifa hizo ni moja ya taarifa ambazo zimekuwa zikisambazwa kwa nia ya upotoshaji. Alisema kwa sasa serikali inawapanga wanafunzi hao na kuchelewa kidogo kutoa majina na shule au vyuo walikopangiwa, kumetokana na utaratibu wa kuwapanga katika mfumo wa Divisheni kutoka mfumo wa GPA.

Majaliwa alisema mwaka huu wanafunzi wengi zaidi wamefaulu kwenda kidato cha tano na serikali pia ilikuwa ikifanya sensa ya shule za kidato cha tano na sita na vyuo vya diploma na uwezo wao, ili wote wapangiwe bila kumuacha hata mmoja.

Aliwahakikishia wabunge, wazazi wa wanafunzi hao na wanafunzi wenyewe, kuwa serikali itatoa majina hayo wiki mbili kabla ya muda wa kwenda kuanza masomo katika shule na vyuo husika, ili kutoa nafasi kwao kujipanga kusafirisha wanafunzi hao.

Katika swali jingine, Mbunge wa Viti Maalumu, Hamida Mohamed Abdallah, alihoji ni vipi Serikali itahakikisha inapeleka fedha kwa wakati katika halmashauri na hivyo kwenda katika miradi ya maendeleo, wakati kuna watendaji wengi wanakaimu nafasi zao?

Akijibu swali hilo, Majaliwa alisema serikali itahakikisha inapeleka fedha zote za maendeleo kama ilivyokusudiwa katika bajeti ya serikali, ambayo asilimia 40 ya fedha zote imeamuliwa kwenda katika maendeleo kutoka asilimia 27 ya bajeti iliyopita.

Alisema ili kufanikisha lengo hilo, serikali imekusudia kuimarisha ukusanyaji wa mapato, kuziba mianya ya ukwepaji wa kodi na kuongeza usimamizi katika miradi itakayopelekewa fedha hizo.

Kuhusu watu kukaimu, ikiwemo wakurugenzi wa halmashauri, Majaliwa alisema Rais John Magufuli bado anaunda serikali yake ambapo kwa sasa eneo lililobaki ni la wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri.

Chanzo: Habari Leo

0 comments