Sunday, 27 August 2017

MAMBO YA KUZINGATIA UNAPOTAKA KUSAFIRI NA MTOTO

By    

Na Jumia Travel Tanzania

Sidhani kama kuna mtu hajawahi kukumbana na kadhia ya watoto kwenye chombo cha usafiri iwe ni basi, meli, ndege, treni au usafiri binafsi. Ni mara ngapi umewahi kusafiri halafu ukaketi pembeni na mtoto ambaye yeye analia tu safari nzima huku mzazi akiwa hana njia yoyote ile ya kumnyamazisha? Nadhani utakuwa una kumbukumbu nzuri tu ya namna ulivyokwazwa.

Zipo sababu nyingi ambazo husababisha watoto kuwa wasumbufu wakiwa njia na kwa kawaida hiyo ni asili yao kutokana na umri au udadisi walionao. Jumia Travel imemekukusanyia mbinu zifuatazo ili kuzuia hali hiyo kutojirudia tena pindi utakasafiri.      


Jipange mapema kwa safari. Maandalizi ni muhimu kwenye jambo lolote lile ili uweze kufanikiwa. Vivyo hivyo kwenye safari yoyote ile inabidi ujipange mapema hususani kama unatarajia kusafiri na watoto wadogo. Yapo mahitaji mengi ya kuzingatia unapokuwa safarini na watoto tofauti ukiwa wewe mwenyewe. Watoto wanahitaji uangalizi na umakini wa hali ya juu. Hivyo basi hakikisha kama haujawahi kusafiri na watoto basi ni vema ukaulizia kwa waliowahi kufanya hivyo ili ujue mambo ya kuzingatia na kutarajia.    

Wasiliana na kampuni unayoarajia kusafiri nayo. Zipo taratibu tofauti zilizowekwa na makampuni mbalimbali ya usafiri pale linapokuja suala la kusafiri na watoto. Kama mzazi unaweza ukafikiri kwamba watoto hawatozwi nauli na mambo yakawa tofauti. Imetokea mara kadhaa unakuta wazazi wanasafiri na watoto wao na wakalazimishwa kuwalipia nauli kama watu wazima. Hivyo ili usije kushtukizwa na jambo hili ni vema ukafanya utaratibu mapema.

Kata tiketi mapema. Baada ya kujipanga na safari yako na kujua taratibu zote za kufuata ni vema ukakata tiketi yako mapema iwe ni basi, meli au ndege. Hii itakuepusha na maandalizi ya dakika za mwisho ambayo yanaweza kukusababishia ukakosa usafiri. Mbali na hapo kukata tiketi mapema kunaweza kukusaidia ukapata kwa bei rahisi na pia kuchagua kuketi mahali utakapopenda wewe. Lakini pia itakupatia muda wa kujipanga na mahitaji mengine pindi ukiwa safarini.  

Beba begi la nguo za watoto. Tofauti na watu wazima kwa watoto wadogo inahitaji kubeba nguo za ziada. Ukiwa njiani mtoto anaweza kujisaidia, kutapikia au kujichafua pindi anakula au unamlisha. Hivyo haitopendeza kusafiri na mtoto safari nzima akiwa mchafu. Katika kuchagua nguo za kubeba hakikisha unabeba zile zilizo muhimu tu ili kuepuka mzigo usiwe mzito.  

Pakia chakula cha njiani kwa ajili ya watoto. Unaposafiri na mtoto mdogo ni vema ukatambua kwamba siku zote yeye huhitaji kile anachokitaka muda na wakati ule ule. Kwa hiyo ili kuepuka usumbufu kwa abiria wengine pale mtoto anapohitaji chakula hakikisha umebeba kwenye begi lako. Mtoto mdogo haelewi kwamba kula ni mpaka mfike kituo fulani au ufike mwisho wa safari. Mara nyingi watoto wakikosa kile wanachokihitaji hulia jambo ambalo huwakera abiria wengi.

Beba vitu vya kuchezea. Kwa kuwa safari nyingi huchukua muda na umbali mrefu kumalizika hakikisha kwenye mizigo yako umejumuisha vitu vya kuchezea au kumtuliza kwa ajili yake. Unaweza kubeba midori anayoipendelea, vifaa vya michezo au vitabu. Vitu hivyo vitasaidia kumtuliza kwa umbali na muda fulani hata kama sio safari yote. Ukiwa na mtoto ambaye hasumbui au hupendelea kulala zaidi basi utakuwa umebarikiwa sana lakini inajulikana watoto wengi ni wasumbufu.

Usisahau kubeba dawa. Kwenye safari mambo mengi hutokea mojawapo ni afya kubadilika ghafla. Huwa inatokea mara kadhaa ukakuta abiria anatoka salama lakini kufika katikati ya safari akaumwa na kichwa, tumbo kuchafuka au kusikia kizunguzungu. Msaada pekee katika kukabiliana na changamoto hizo ni kubeba dawa. Na kwa mtoto pia hakikisha unamuona mtaalamu wa kiafya ili kupata ushauri juu ya changamoto gani zinaweza kumkumba mtoto safarini na namna ya kukabiliana nazo.

Kama mdau wa huduma za usafiri kwa njia ya mtandaoni ndani na nje ya Tanzania, Jumia Travel inatarajia kuzindua vifurushi ambavyo vitalenga wanafamilia. Kupitia huduma hii mpya itakayozinduliwa hivi karibuni, wanafamilia hawatokuwa tena na wasiwasi juu ya kusafiri na watoto wao ambapo mara nyingi huwa ni changamoto kubwa. Kwani kupitia ushirikiano na maelefu ya hoteli wanayoshirikiana nayo nchi nzima wamelirahisisha suala hilo kwa kutenga gharama nafuuu kabisa.

0 comments