Wednesday 19 June 2013

NGONO KWA NJIA YA MDOMO HUSABABISHA KANSA !

Photo

Mapenzi

Saratani imeendelea kuwa tishio hapa nchini huku hofu ikiendelea kuikumba jamii kutokana na wataalamu wa afya kushindwa kufahamu tiba halisi ya maradhi hayo hatari.

Takwimu kutoka Taasisi ya Saratani ya Ocean Road zinaonyesha ongezeko la saratani ya mdomo na koo kwa kiasi kikubwa kutoka kesi 167 mwaka 2006 hadi 277 mwaka 2012.

Mkurugenzi wa Idara ya Kinga Ocean road, Julius Mwaiselage anaeleza kuwa watanzania wasipende kuiga mambo ambayo si sahihi bila kujua madhara yake kama kufanya mapenzi kwa njia ya mdomo. “Saratani ya mdomo ipo, na nyingine zinasababishwa na zinaa “ anasema Dk Mwaiselage

Tafiti mbalimbali zimewahi kufanyika nchini na kubaini kuwepo kwa ongezeko la saratani ya mdomo.Utafiti uliofanywa na Dk Innocent Mosha wa Kitengo cha Patholojia cha Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), umebaini aina za saratani 1,594, kati ya hizo 509 zikiwa ni za midomo kwa mwaka 2003 pekee.

Matokeo hayo yanaonyesha kuwa kati ya saratani 509 za mdomo, saratani 242 zilisababishwa na Virusi vya Human Papiloma ambavyo hutokana na zinaa.

“Ninachojua mimi ni kuwa Virusi vya HPV husababishwa na magonjwa ya zinaa, hivyo mtu anayeugua saratani ya aina hiyo, imetokana na zinaa,” anasema Dk Mosha.

Takwimu hizo ni zile zilizopatikana kwa watu waliokwenda kufanyiwa uchunguzi katika Mkoa wa Dar es Salaam pekee.

Dk Mosha anasema kuwa wanaume ndiyo huathiriwa zaidi na saratani ya mdomo ambapo kwa hapa nchini, asilimia 53 ya wanaume waliofika MNH kwa ajili ya vipimo, walibainika kuugua saratani hiyo, huku wanawake wakiwa ni asilimia 47.

Utafiti kama huo ulifanywa pia na Dk Amos Mwakigonja, mkuu wa Idara ya Patholojia katika Chuo Kikuu cha Tiba cha Muhimbili (MUHAS).

Dk Mwakigonja alifanya utafiti wa saratani ya mdomo aina ya Kaposi’s Sarcoma ambapo wagonjwa 78 walibainika na saratani hiyo kuanzia mwaka 1990 hadi 2003. “Saratani za mdomo zipo za aina nyingi na zimetofautiana kulingana na visababishi vyake,” anasema Dk Mwakigonja.

Katika utafiti wake Dk Mwakigonja alibaini kuwa wanawake wengi walikuwa na saratani ya mdomo aina ya Kaposi’s Sarcoma kuliko wanaume.

Hata hivyo, utafiti huo ulionyesha kuwa asilimia 50 ya wanaume walikuwa na saratani ya mdomo hatari zaidi (systemic) kuliko wanawake ambao ni asilimia 37.

Mapenzi kwa mdomo husababisha maradhi


Dk Mwakigonja anasema kuwa mapenzi yoyote kwa njia ya mdomo lazima yasababishe maradhi ya zinaa iwapo mmoja ameambukizwa.

Pia anasema kwamba sampuli nyingi za wanaume wanaojihusisha na mapenzi na wanaume wenzao (mashoga) zilibainika na saratani ya mdomo.

Utafiti huo ni sehemu ya utafiti wa Shahada ya Uzamivu ambao ulionyesha kuwa wagonjwa wengi wa saratani ya mdomo walikuwa ni wanaume wenye umri wa miaka kati ya 38 na kuendelea na wanawake ni 31.

Ufatiti wa WHO Tanzania


Shirika la Afya Duniani (WHO) pia lilifanya utafiti mwaka 2010 nchini kwa kushirikiana na Kituo cha Taarifa za HPV, ambapo ilibainika kuwa asilimia 20 ya saratani za koo na mdomo nchini zinasababishwa na ufanyaji wa mapenzi kwa njia ya mdomo.

Taarifa hizo za WHO zinaeleza kuwa wanaume 747 hugundulika na saratani ya mdomo kila mwaka wakati wanawake 472 hubainika na saratani hiyo pia.

Wakati huohuo, wanaume wanaopoteza maisha kutokana na saratani hiyo ni 444, kwa mwaka na wanawake ni 270, kwa mwaka.

Utafiti wa WHO umebaini kuwa saratani ya mdomo inashika nafasi ya sita katika aina 24 za saratani 24 zinazoisumbua zaidi Tanzania.

Ripoti hiyo inaeleza kuwa wanaume wanaoathirika zaidi ni wenye umri wa kati ya miaka 15 na 55, ambao tayari wameshaanza kujihusisha na ngono.

Kama maradhi mengine ya kuambukiza, Virusi vya HPV huambukizwa kwa urahisi zaidi kutoka kwa wanawake kwenda kwa wanaume kuliko kutoka kwa wanaume kwenda kwa wanawake.

Utafiti huo uliodhaminiwa na mfuko wa Bill na Melinda Gates na Kituo cha Saratani na Mpango wa Utafiti wa Taasisi ya ICO unaeleza kuwa mitandao ya kijamii na picha za ngono ndiyo chanzo cha watu wengi kuiga ufanyaji wa mapenzi ya aina hiyo.

Kwa mujibu wa gazeti la The New York Times, tafiti zimefanyika na kubaini kuwa asilimia 70 ya wagonjwa wanaobainika na saratani ya koo na mdomo duniani, husababishwa na Virusi vya Human Pappiloma vinavyotokana na magonjwa ya zinaa.

Tafiti hizo zinaonyesha kuwa wagonjwa wengi wanaogundulika na saratani hiyo ni wanaume wenye umri wa kati, wenye uwezo wa kifedha, wasiovuta sigara wala siyo walevi waliokubuhu.

Utafiti huo ulibaini kuwa wanaume wapo hatarini zaidi kupata saratani ya koo inayosababishwa na Virusi vya HPV.

Miaka ya 80, idadi ndogo ya watu waliougua saratani ya koo walihusishwa na maambukizi ya Virusi vya HPV.

Kihistoria, watu waliobainika na ugonjwa huo, ni wenye umri wa miaka 70 kwenda juu ambao walikuwa ni wale walevi waliokubuhu na wavuta sigara.

Ilielezwa kuwa Virusi vya HPV vipo kwa wingi kiasi ambacho watu wazima wanaojihusisha na ngono ya aina yeyote ile, huweza kupata maambukizi ya zinaa hata kama siyo saratani.

Hata hivyo ilibainishwa kuwa saratani isababishwayo na virusi vya HPV ni rahisi kuitibu kuliko saratani ya koo isababishwayo na tumbaku au pombe kali.

Virusi vya HPV ni nini?


Kwa jina la jumla, saratani ya koo au mdomo huitwa saratani ya kichwa na shingo. (Neck and Head Cancer)

HPV ni miongoni mwa virusi hatari zaidi duniani visababishwavyo na magonjwa ya zinaa na vinaweza kuathiri sehemu mbalimbali za mwili.

Zipo aina zaidi ya 120 za HPV, baadhi huweza kuzalisha usugu (warts) ambazo si saratani katika sehemu za siri, mikononi na miguuni.

Maambukizi ya HPV hufanyika kwa urahisi, hata kwa kugusana ngozi au majimaji, huku maambukizi mengine yakisababishwa na ngono.

Virusi hatari na vinavyosababisha saratani ni HPV-16, HPV-18, HPV-31 na HPV 45.
Aina hii ya Virusi vya HPV husababisha saratani ambapo uvimbe waweza kujitokeza kwa ndani na unaweza usionekane ukilinganisha na vivimbe vingine vya saratani.

 Wataalamu wanasema HPV-16 na HPV-18 inahusishwa zaidi na saratani ya shingo ya kizazi na endapo mapenzi kwa njia ya mdomo yatafanywa na mtu mwenye uambukizo huu ni rahisi kuambukizwa

0 comments