UTANGULIZI
Ndugu Wananchi, wanachama na viongozi wa CHADEMA,
Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) iliyokutana
Ubungo Plaza, Dar es Salaam kuanzia asubuhi ya siku ya Jumatano ya
tarehe 20 Novemba, 2013 hadi alfajiri ya leo Ijumaa tarehe 22 Novemba,
2013 imetafakari na kujadili kwa kina taarifa mbali mbali juu ya hali ya
kisiasa ndani na nje ya Chama chetu ambayo kwa muda mrefu imegubikwa na
tuhuma kubwa na nzito dhidi ya Chama chetu na viongozi wake wakuu,
yaani Mwenyekiti wa Taifa, Mheshimiwa Freeman Aikaeli Mbowe (MB), na
Katibu Mkuu, Dk. Wilbrod Peter Slaa. Tuhuma hizi zilikuwa na malengo na
athari ya kuwapaka matope na kuwachafua viongozi wakuu wa Chama na Chama
chenyewe, kutengeneza mtandao wa siri ndani na nje ya Chama ambao
hatimaye ungefanikisha sio tu lengo la kufanya mapinduzi nje ya
utaratibu wa kikatiba wa Chama, bali pia ungekipasua Chama vipande
vipande na hivyo kuua matumaini ya Watanzania juu ya uwezekano wa
kufanya mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi na kijamii katika nchi yetu
kwa kukiondoa madarakani Chama cha Mapinduzi (CCM).
Ndugu Wananchi, wanachama na viongozi wa CHADEMA,
Uchunguzi wa Kamati Kuu umebaini kuwepo kwa mkakati mkubwa wa kutimiza
malengo hayo ambao umeandikwa katika waraka unaoitwa ‘Mkakati wa
Mabadiliko 2013.’ Mkakati huu uliandaliwa na kikundi kinachojiita
‘Mtandao wa Ushindi’ ambacho vinara wake wakuu ni wanne, yaani Naibu
Katibu Mkuu na Naibu Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni,
Mheshimiwa Zitto Zuberi Kabwe ambaye kwenye waraka huo anajulikana pia
kama ‘MM’ au ‘Mhusika Mkuu’; mjumbe wa Kamati Kuu na mwanazuoni kutoka
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Kitilla Mkumbo ambaye kwenye waraka
anajulikana pia kama M1; Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Arusha ambaye kwa
sasa amesimamishwa uongozi, Bwana Samson Mwigamba na ambaye kwenye
waraka anaitwa M3; na mtu mwingine ambaye hadi sasa jina lake
halijajulikana lakini kwenye waraka anajulikana kama M2 na anatajwa kuwa
yuko ‘ukingoni kupigwa nje’ katika mageuzi ya kiutendaji yanayoendelea
katika Sekretariat ya Chama hapa Makao Makuu.
Kwa mujibu
wa waraka wenyewe, “Mkakati huu umeandaliwa kwa pamoja na M2 na M3 na
kupitiwa na kurekebishwa na M1 ili upelekwe kwa MM kwa maoni ya mwisho
na kuanza utekelezaji.” Mbele ya Kamati Kuu, Dk. Mkumbo alikiri kwamba
MM au Mhusika Mkuu ni Naibu Katibu Mkuu Zitto Kabwe; M1 ni yeye mwenyewe
Dk. Mkumbo na M3 ni Bwana Mwigamba. Dk. Mkumbo alikataa kata kata
kumfahamu M2. Aidha, Dk. Mkumbo alikiri mbele ya Kamati Kuu kwamba yote
yaliyoandikwa katika ‘Mkakati wa Mabadiliko 2013’ yametoka kwenye
‘Mtandao wa Ushindi’ na hayajabadilishwa.
Ndugu Wananchi, wanachama na viongozi wa CHADEMA,
Mkakati wa Mabadiliko 2013 ni mpango wa kuipasua pasua CHADEMA na
kuiangamiza kabisa kwenye uso wa siasa za Tanzania. Huu sio mkakati wa
kufanya mabadiliko ya kiuongozi ndani ya Chama kwa njia za kidemokrasia
na za kikatiba. Ni mpango wa kukiteka nyara Chama na kukiua. Ndio maana
watunzi wa waraka huu wamesema kwenye waraka wao: “Tunahitaji kutekeleza
mkakati huu kwa siri kubwa ili mkuu aliyepo aendelee kubweteka na ndio
maana hata lugha iliyotumika ndani hapa ni ya pekee.” Kamati Kuu
inaamini mkakati wenye malengo halali ya kufanya mabadiliko ndani ya
Chama kwa njia halali za kikatiba usingependekeza
kwamba: “Vikao vyetu na yeye (MM aka Mhusika Mkuu aka Naibu Katibu Mkuu
Zitto Kabwe) vitafanyika mara chache sana na mahali pa faragha kupita
kiasi ikiwezekana hata nchi jirani.” Aidha, Kamati Kuu inaamini kwamba
kama mkakati huu ungekuwa na malengo mazuri ya kukijenga Chama na sio
kukiteka nyara na kukiua, wanamtandao hawa wasingependekeza
utaratibu ufuatao wa utekelezaji wa mpango: “M1 (Dk. Mkumbo) ndiye
atakayekuwa anawasiliana na tunayemtaka ambaye ataitwa MM (Mhusika
Mkuu). Tumepanga kwamba kusiwe na mawasiliano mengi kati ya kamati na
mhusika mkuu kuepuka tracking ya wapinzani wetu. M1 ni mtu wa karibu na
MM kwa hiyo mawasiliano yao hayataweza kutiliwa shaka na mtu yeyote hata
wangewasiliana mara nyingi kiasi gani. Hata hivyo, linapokuja suala la
mkakati huu tunasihi mawasiliano yawe kwa kuonana uso kwa uso ama kwa
simu na si sms. M1 ndiye atakayewasilisha
mambo yote yanayotoka kwenye kamati ya kitaifa na endapo kuna haja ya
MM kukutana na kamati ya kitaifa, mipango yote ya kikao itafanywa na M1
kwa usiri mkubwa.”
Ndugu Wananchi, wanachama na viongozi wa CHADEMA,
Mkakati wa Mabadiliko 2013 ni mpango haramu na ambao unaichana chana
Katiba ya Chama chetu. Ni mkakati wa vita dhidi ya Chama chetu na
utaratibu wetu wa kikatiba.
Wakati ibara ya 10.1(iv) ya Kanuni
za Uendeshaji Kazi za Chama ambazo ni sehemu ya Katiba ya Chama chetu ya
mwaka 2006 inamkataza kiongozi wa CHADEMA asijihusishe na vikundi
vyenye misingi ya ukabila, udini, au ukanda ambavyo vina makusudi ya
kubaguana ndani ya Chama na miongoni mwa jamii kisiasa au kijamii”,
wanaMtandao wa Ushindi wameonyesha wazi kuwa wanaendekeza siasa za udini
kwa kusema yafuatayo juu ya waliemwita ‘mtu tunayemtaka’, yaani Naibu
Katibu Mkuu Zitto Kabwe: “Kwa kuwa ni Mwislamu, hii ni fursa katika
kupata kuungwa mkono na wanachama waislamu ambao wamekuwa na kigugumizi
wakidhani waislamu hawatakiwi katika uongozi wa taasisi yetu.”
Wakati ibara ya 10.1(viii) ya Kanuni za Uendeshaji inamtaka kila
kiongozi wa CHADEMA “... kuwa mkweli na muwazi wakati wote ... na
aachane na vikundi vya majungu na wadanganyifu (rumour mongers) ...”,
wanaMtandao wa Ushindi wameeleza kwenye waraka wao kwamba mipango yao ya
utekelezaji wa Mkakati wa Mabadiliko 2013 ‘itafanyika kwa usiri
mkubwa.’
Wakati ibara ya 10.1(ix) ya Kanuni za Uendeshaji Kazi za
Chama inamtaka “kiongozi asijihusishe na vikundi na vitendo vya
kuchonganisha au kuzua migogoro ndani ya uongozi wa chama au wanachama
wake”, wanaMtandao wa Ushindi wamesambaza tuhuma za uongo dhidi ya
Mwenyekiti wa Chama Taifa (ambaye wanamwita kwenye waraka wao kuwa ni
‘Mpinzani wetu’) kuwa “... hana mahusiano mema na mazuri na viongozi wa
ngazi za chini kutokana na dharau nyingi anazozionyesha pale anapokutana
na viongozi wa ngazi za chini akiwa katika kuijenga taasisi hii.... Hii
imemfanya kutopendwa na viongozi wengi wa ngazi za chini hivi sasa na
kutoa fursa ya pekee kwa tunayemtaka.”
Wakati ibara ya 10.1(x) ya
Kanuni za Uendeshaji inamtaka “kiongozi asitoe tuhuma zozote juu ya
viongozi wenzake pasipo kupitia vikao halali na kuzingatia taratibu na
ngazi zilizowekwa kwenye Kanuni”, tuhuma zote zilizotolewa na
wanaMtandao hawa dhidi ya viongozi wakuu wa Chama chetu hazijawahi
kutolewa na yeyote kati ya wanaMtandao hawa katika kikao chochote halali
cha Chama cha ngazi yoyote.
Wakati ibara ya 10.1(xii) ya Kanuni za
Uendeshaji inaeleza kwamba “itakuwa marufuku kwa kiongozi wa CHADEMA
kukashifu Chama, kiongozi au mwanachama yeyote wa Chama ...”, Mkakati wa
Mabadiliko 2013 umejaa kashfa kubwa, matusi mengi na udhalilishaji
mkubwa wa Chama, viongozi wake wakuu na wanachama kwa ujumla. Hivyo, kwa
mfano, Mwenyekiti wa Chama Taifa ametuhumiwa na wanaMtandao hawa kuwa
ni mtu mwenye ‘uzalendo unaotia shaka’, mwenye ‘elimu ya magumashi’,
‘mzito kujieleza’, ‘mtu mwenye akili ndogo’, n.k.
Ndugu wananchi, wanachama na viongozi wa CHADEMA,
Hakuna chama au taasisi yoyote duniani inayoweza kunyamazia mkakati wa
aina hii dhidi yake na viongozi wake wakuu na ikadumu au kubaki salama.
Chama au taasisi yoyote inayoendekeza vitendo vya aina hii miongoni mwa
viongozi wake wa ngazi yoyote au miongoni mwa wanachama wake wa kawaida
inakaribisha kifo na mauti. Chama chetu na viongozi wake wa juu wamekaa
kimya kwa muda mrefu sana; wamevumilia mashambulizi na kashfa nyingi
sana dhidi yao binafsi na dhidi ya Chama; wamestahimili matusi makubwa
sana dhidi yao. Chama chetu kimevumilia yote haya na viongozi wake
wamevumilia yote haya sio kwa sababu walitaka Chama chetu kiuwawe na
wanaMtandao hawa. Uvumilivu wote huu ulitokana na haja ya kuwapa
wanaMtandao wa Ushindi fursa ya kugundua hatari ya siasa zao na kuwapa
muda wa kujirekebisha na kujirudi.
Kama ilivyo kwa
binadamu au taasisi yoyote ile, uvumilivu wa Chama chetu na viongozi
wake wakuu una kikomo. Na hiki ndio kikomo cha uvumilivu wa Chama chetu,
viongozi wake na wanachama wake kama wanavyowakilishwa
na Kamati Kuu ya Chama chetu. Hivyo basi, katika kikao chake tajwa,
Kamati Kuu ya Chama chetu, kwa kutumia mamlaka yake ya kikatiba ya
dharura chini ya ibara ya 6.5.2(d) ya Katiba ya Chama, imeazimia
yafuatayo kuhusu Mkakati wa Mabadiliko 2013 na hao wanaojiita
wanaMtandao wa Ushindi:
Kwamba, kuanzia sasa, viongozi wote
waliohusika ama kuhusishwa na mkakati huu, yaani Naibu Katibu Mkuu Zitto
Kabwe, Mjumbe wa Kamati Kuu Dk. Kitilla Mkumbo na Mwenyekiti wa Mkoa wa
Arusha Samson Mwigamba wavuliwe nyadhifa zao zote za uongozi ndani ya
Chama;
Kwamba timu ndogo ya pamoja ya watendaji wa Sekretariat ya
Makao Makuu ya Chama na wajumbe wa Kamati Kuu ifanye uchunguzi wa haraka
ili kumtambua mtu anayeitwa M2 na ambaye anadaiwa kuwa mtumishi wa
Makao Makuu ya Chama ili hatua stahiki na za haraka zichukuliwe dhidi
yake, pamoja na watu wengine wote watakaobainika kuhusika na mpango huu
wa uhaini dhidi ya Chama chetu;
Kwamba Kamati ya Chama ya Wabunge
inaelekezwa kuchukua hatua za haraka za kuhakikisha Naibu Katibu Mkuu
Zitto Kabwe anavuliwa madaraka yake yote kama Naibu Kiongozi wa Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni, with immediate effect;
Kwamba viongozi
waliotajwa katika aya ya (a) waandikiwe hati zenye tuhuma dhidi yao
haraka iwezekanavyo na watakiwe kujieleza kwa nini wasifukuzwe kwenye
Chama kwa vitendo vyao na wapatiwe fursa kamili ya kujitetea kama
inavyotakiwa na ibara ya 6.5.2(a), (b) na (c) ya Katiba ya Chama;
Kwamba mara baada ya utekelezaji wa azimio (d), Kamati Kuu ikutane kwa
dharura kwa ajili ya kufanya uamuzi juu ya hatma ya watuhumiwa na hatua
nyingine zitakazofuata;
Kwamba waraka wa wanaojiita wanaMtandao wa
Ushindi uwekwe hadharani na usambazwe kwa vyombo vya habari vya aina
zote ili wananchi wa Tanzania, wanachama na viongozi wa Chama chetu na
dunia nzima kwa ujumla iweze kupima uzito wa Mkakati wa Mabadiliko 2013
na uhalali wa maamuzi haya ya Kamati Kuu.
Ndugu wananchi, wanachama na viongozi wa CHADEMA,
Naibu Katibu Mkuu Zitto Kabwe na Mjumbe wa Kamati Kuu Dk. Kitilla
Mkumbo waliiomba Kamati Kuu iwaruhusu kujiuzulu nyadhifa zao baada ya
Mkakati wao wa kukiteka nyara Chama na kukiangamiza kujulikana mbele ya
Kamati Kuu. Kwa kuzingatia uzito wa makosa waliyokifanyia Chama,
viongozi wake wakuu na wanachama wake kwa ujumla; na kwa kuzingatia
uzito na umuhimu wa nyadhifa kubwa walizo nazo ndani ya Chama; na kwa
kuzingatia uelewa wao wa Katiba, Kanuni na taratibu za Chama na uzoefu
wao katika safu za juu za uongozi wa Chama, Kamati Kuu ilikataa kwa
kauli moja kuridhia maombi hayo ya kujiuzulu. Kufanya hivyo ingekuwa ni
sawa na kuwaruhusu wajiondoe kwenye uongozi wa Chama wakiwa na heshima
wasizostahili hata kidogo.
Chama chetu ni tumaini pekee la
Watanzania wote wanaotaka mabadiliko ya kweli na ya kimsingi katika
mfumo wa kiutawala, kiuchumi na kijamii wa nchi yetu. Hii ndiyo sababu
kubwa na ya pekee iliyosababisha vita kubwa na chafu inayopigwa dhidi ya
Chama chetu na viongozi wetu wakuu. Lengo kuu ni kuwachafua viongozi
wakuu, kuleta mgogoro na mgawanyiko ndani ya wanachama, viongozi wake na
hivyo kukichafua Chama mbele ya macho ya Watanzania. Chama chetu
kikishachafuka kwa mtindo huu, matumaini ya Watanzania wanaotaka
mabadiliko yatakufa. Vita hii kubwa haijaanza jana, na haitaisha kesho.
Kama ambavyo tumekabiliana nayo na kuishinda siku za nyuma, vivyo hivyo
tutakabiliana nayo mara hii na kuishinda. Kama Chama chetu kilivyoibuka
na nguvu na heshima kubwa zaidi katika mapambano ya siku za nyuma, vivyo
hivyo Chama chetu kitaibuka na nguvu na heshima kubwa zaidi katika
awamu hii ya mapambano.
Tunawaomba Watanzania, wanachama na
viongozi wetu wasife moyo, bali waendelee kukiunga mkono chama chao cha
ukombozi. Tunawaomba Watanzania, wanachama na viongozi wetu waendelee
kulilinda tumaini lao pekee la mabadiliko ya kisiasa, kiuchumi na
kijamii katika nchi yetu. Badala ya kukatishwa tama, kila mmoja wetu
aongeze bidii maradufu ili kuwashinda wale wanaotaka kuleta majanga
katika Chama chetu na kwa Taifa letu.
------------------------------------------
FREEMAN AIKAELI MBOWE (MB) - MWENYEKITI, TAIFA
------------------------------------------
WILBROD PETER SLAA
KATIBU MKUU
0 comments