NA EDO KUMWEMBE
WAKATI mwingine hakuna unachoweza kufanya zaidi
ya kucheka. Hata kama haucheki usoni. Unacheka moyoni na kujiuliza, ni
namna gani Kigogo anayehusika na wizi wa Meno wa Tembo anavyokandia
uwezo wa Mrisho Ngassa.
Ndio, unakutana na Mbunge Kigogo. Jina lake
linatajwa katika wizi wa Meno ya Tembo. Anakwambia “Hivi Edo unataka
kuniambia niache kushangilia Manchester nije kutazama Taifa Stars.
Hatujui mpira sisi Watanzania”. Moyoni namjibu, kweli hatujui mpira,
lakini kulinda Rasilimali zetu kama Meno ya Tembo unayoiba ndio
tumeweza?
Unajiuliza, sawa sisi hatujui mpira, lakini tumefanikiwa
katika nini hasa? Barabara? Madini? Kilimo? Siasa? Elimu? Hapana.
Hatimaye tumefika katika nyakati ambazo Taifa kama Taifa limekwama. Ni
kitu gani kingine cha kujivunia wakati unapoponda soka la Tanzania?
Hakuna.
Aliyempa tenda mkandarasi mbovu kujenga barabara mbovu ya
Kilwa, naye anauponda mpira wa Tanzania. Aliyesaini mkataba mbovu wa
Madini ambao unaruhusu Mzungu kuchota Madini yetu atakavyo, naye
anamponda kocha wa Taifa Stars na wachezaji wake.
Anayeongeza sifuri
katika hesabu ya safari za Rais Ulaya naye akikutana na Watanzania
wanaoshi nje anauponda mpira wa Tanzania. Yeye ni Mwizi mzuri tu, lakini
wala haoni hesabu za wizi wake zinavyoshindwa kusomesha walimu wa soka
nje ya nchi.
Umewahi kumsikia Mbunge wa kile Chama akiponda
wachezaji wa Tanzania? Lakini ndiye huyo huyo aliyegonga meza na wenzake
kupitisha bajeti ya Wizara ya Elimu na Michezo na wakaipa shilingi 600
milioni. Huo ni mshahara wa wiki moja wa mchezaji anayetoka nchi ya
Afrika anayecheza Ulaya, Yaya Toure. Bajeti hii ya mshahara wa wiki wa
Yaya Toure inainuaje soka?
Anayepaswa kutatua tatizo la foleni jiji
la Dar es salaam akashindwa na kujiongezea posho za kijinga kila siku
naye analaumu matokeo mabovu ya timu ya Taifa na viwango vibovu vya
Simba, Yanga, Azam katika michuano ya Caf.
Kigogo wa TRA ni shabiki
mzuri wa Arsenal. Anamsaidia yule Mfanyabiashara maarufu kukwepa kodi.
Hajui kwamba pesa tunayopoteza ingesaidia uchumi wa nchi na michezo wa
ujumla. Hapa huwa ananiacha hoi kweli kweli.
Lakini anauchekaje
mchezo wa soka? Kama mchezo wa soka umefeli, kwani hajui ni kwa kiasi
gani Tanzania imefeli katika kukusanya kodi nyingi miongoni mwa nchi za
Afrika? Hapa si ndio nchi ambayo Mfanyabiashara anapewa miaka mitano ya
kutolipa kodi mpaka ajue faida ya biashara yake? Wenyewe wanaita kwa
kizungu Tax Holiday.
Kigogo wa Wizara nyeti ya ulinzi anamlinda
Kigogo mwenzake aliyebaka mtoto wa kiume. Wakiimaliza kesi kituo cha
Polisi wanaitana Serena Hoteli kupongezana kwa kula mishkaki huku
wanacheki mechi ya Taifa Stars dhidi ya Ivory Coast TBC. Tukifungwa
wanasema hatujui mpira na wachezaji wetu ni duni.
Unajiuliza, kwani
mchezaji wa Tanzania si anatokana na mtoto wa Kitanzania? Mbona wametoka
kumkandamiza mtoto wa Kitanzania? Naishia kucheka taratibu kwa uchungu.
Mchezaji mwenye kipaji kama Haruna Moshi ‘Boban’ hajaweza kung’ara
Ulaya. Kuna tofauti gani na Mlima Kilimanjaro kushindwa kusaidia uchumi
wa Taifa lake zaidi ya ilivyo sasa. Kuna tofauti gani na Mtanzania kufa
njaa wakati ana ardhi kilomita nyingi zenye rutuba?
Mwisho wa yote
tunaishi katika Taifa lililooza. Taifa lisilo na maadili katika uchumi,
jamii na siasa. Kila unapowaza unakubali kwamba soka la Tanzania lipo
chini na limeoza. Hatuonyeshi matumaini. Lakini niambieni ni wapi kuna
matumaini na nidhamu?
Tatizo limebaki kwa Mtanzania mwenyewe.
Hana uzalendo, ubunifu na umakini. Niambieni ni nani halaumiwi?
Mwandishi wa habari? Mchezaji? Polisi? Rais? Mbunge? Mwanajeshi?
Daktari? Mmachinga? Mfanyabiashara? Mkulima? Kila mtu haifanyi kazi yake sawa sawa.
Ni kweli. Tumekosa dira kama taifa. Hatujui tulipo wala tunapokwenda.
Kabla haujamlaumu mwenzako jiulize, wewe unaifanyia nini nchi yako. je
wewe Sekta yako ina maendeleo yanayostahili kabla ya kumnyooshea kidole
mwingine?
Huwa nawaza sana. Daktari aliyemfanyia operesheni ya
kichwa mtu anayestahili kufanyiwa operesheni ya goti, naye anamlaumu
Polisi aliyechukua rushwa jana Kariakoo. Na yule polisi naye analaumu
matokeo mabovu ya timu ya taifa. Na hata wachezaji wa timu ya taifa
wanalalamika kuwa Rais anaendesha nchi hovyo. Rais naye ana malalamiko
yake mengi kwa wananchi wa Mtwara kukataa gesi kutoka kusini.
kila
mtu anamlaumu mwingine. Cheni ya lawama inakuwa ndefu, lakini mwisho wa
siku ukweli unabakia pale pale kwamba Taifa limekosa maadili. Nani yuko
salama na nani anafanya kazi yake kwa maadili makubwa?. Hakuna.
Kigogo anayeongoza Bandari anajifanya analaumu kwanini wachezaji wa
Tanzania hawachezi Ulaya. Wala hajiulizi kwanini chini ya Bandari yake
uchumi wa Tanzania usiongoze Afrika Mashariki na kati na baadhi ya nchi
za Ulaya zisizo na Bandari.
Wabrazil wanakosea kwingine, lakini
mpira wanajua. Wachina wanakosea katika mpira, lakini uchumi wanajua.
Wamarekani wanakosea katika moja kidogo, lakini jingine wanafahamu.
Ethiopia wana umaskini, lakini katika riadha wanapatia. Katika soka
wanajitokeza.
Tanzania tunafahamu nini zaidi? Tumepatia wapi hadi
tuseme mpira ni tatizo sana? wasomi na wananchi wa kawaida tuanze
kuitafakari nchi kwa pamoja. Tusitafakari kwa mapande mapande. Tuna
tatizo kila sehemu. Nani hajawahi kulaumiwa au kulaumu? Kila mtu tatizo
nchi hii…
0 comments