Jeshi la Polisi nchini Kikosi cha Usalama Barabarani limewafukuza kazi
askari 27 baada ya kubainika kujihusisha na vitendo vya rushwa ikiwa ni
sehemu ya mkakati wa kuongeza nidhamu, uwajibikaji na maadili ya kazi
kwa askari polisi wa barabarani nchini.
Askari hao wamefukuzwa
kazi kuanzia Januari mwaka huu ambapo uamuzi huo ni sehemu ya
utekelezaji wa usimamizi wa nidhamu na mapambano dhidi ya rushwa baada
ya baadhi ya askari wa jeshi hilo kudaiwa kujihusisha zaidi na vitendo
hivyo.
Ni katika mkutano na waandishi wa habari ndipo Kamanda
wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani Mohamed Mpinga anasema usimamizi
huo dhidi ya vitendo vya rushwa umesaidia ongezeko la ukamataji wa
makosa na mabadiliko ya nidhamu za madereva kwenye matumizi ya barabara.
Akatoa tathmini ya ajali za barabarani na kubainisha Mikoa
iliyoongoza kwa ajali nyingi kuanzia Januari mwaka huu ni Dar Es Salaam
yenye ajali 5,052 Morogoro ajali 514 huku Kilimanjaro ikiwa na ajali
332.
Hata hivyo hali ya ukamataji wa makosa kwa madereva
wasiopenda kutii sheria bila shuruti yameongezeka kulinganisha na mwaka
jana ambapo Januari hadi Juni mwaka huu yamebainika makosa 515,677 huku
Januari hadi Juni mwaka jana yakiwa 301,404 ikiwa ni ongezeko la makosa
214,273 sawa na asilimia 71.
Mwisho.
0 comments