Tuesday, 15 July 2014

MRADI WA MIL 700/- WA MATUMIZI YA RASILIMALI ENDELEVU USAMBARA WAANZA

DSC_0008
Afisa Mradi wa uchumi wa kijani ndani ya hifadhi hai (GEBR) Kitengo cha Sayansi kutoka UNESCO na mwakilishi wa KOICA, Myoung Su Ko, (kulia) akisalimiana na Mtendaji wa Kata ya Mnyuzi, Bw. Gosbert Ishengoma mara baada ya kuwasili kwenye ofisi za kata hiyo wilayani Korogwe. Katikati ni Afisa Usafi na Mazingira wa Wilaya ya Korogwe, Bw. Frederick Linga.
Na Mwandishi wetu, Korogwe
Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) limezindua mradi wa mamilioni katika eneo la hifadhi Usambara Mashariki, kwa mafunzo kwa wakazi waliomo na wanaozunguka hifadhi ya Usambara Mashariki.
Mradi huo ambao umelenga kuwainua wanavijiji kiuchumi huku wakitunza mazingira umepata fedha kutoka Shirika la Ushirikiano wa Maendeleo la Kimataifa la Korea ( KOICA).
Mradi huo unaotekelezwa katika vijiji 19 vinavyozunguka Hifadhi Hai ya usambara mashariki ikiwa ni utekelezaji wa mradi wa uchumi wa kijani ndani ya hifadhi hai(GEBR).
Mradi huo utawawezesha wananchi kwenye vijiji hivyo kutumia raslimali zao kwa namna endelevu. Mradi huo unaojulikana kama “Green Economy in Biosphere Reserves (GEBR)”,wenye thamani ya shilingi milioni 700 utapunguza ukataji miti na kulinda hifadhi kwa kutumia raslimali kwa busara zaidi.
Mradi huo unatarajiwa kuwezesha wananchi wa maeneo hayo kupunguza umaskini kwa kutumia raslimali zilizopo kwa busara na wakati huo huo kuhifadhi mazingira.
DSC_0012
Afisa Mradi wa uchumi wa kijani ndani ya hifadhi hai (GEBR) Kitengo cha Sayansi kutoka UNESCO na mwakilishi wa KOICA, Myoung Su Ko, akisaini kitabu cha wageni kwenye ofisi za kata ya Mnyuzi mara baada ya kuwasili wilayani hapo kwa ajili ya kuzindua mradi wa mamilioni katika eneo la hifadhi Usambara Mashariki, na kuendesha mafunzo kwa wakazi waliomo na wanaozunguka hifadhi ya Usambara Mashariki.
Baadhi ya shughuli zitakazofanyika katika mradi huo ni mafunzo ya kuwawezesha wananchi kufanya shughuli za kiuchumi katika hifadhi ambayo yalifunguliwa leo na Mjumbe wa Kamati ya Hifadhi Hai Tanzania, Joseph Kigula.
Mafunzo hayo kwa vijiji vitatu ambayo yanaendeshwa na EUBR na Wizara ya Mali Asili na Utalii wanavijiji watafunzwa masuala ya menejimenti ya biashara, soko, uhasibu, fedha, ujasiriamali mazingira na elimu ya hifadhi.
Elimu hiyo inatarajiwa kupanua uelewa wanakijiji kuhusu mahusiano ya biashara na hifadhi ya mazingira na kujenga uwezo wa ujasairiamali.
Mafunzo mengine mawili yanatarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwaka.
Mmoja wa wajasirimali, Jason J Drew alisema kwamba mazingira yamekuwa yakiathirika sana katika shughuli za kiuchumi na watu kuachana na dhana ya hamsini kwa hamsini.
UNESCO imesema ni matumaini yake kwamba katika mradi huu, mazingira ya maeneo hayo yataendelea kuneemeka huku wananchi wakifanya shughuli za kiuchumi.
DSC_0023
Baadhi ya wanakijiji wa kata ya Mnyuzi wakitoa burudani kabla ya ufunguzi rasmi wa mafunzo hayo yaliyoanza jana kwenye hoteli ya SB Palace kata ya Mnyuzi wilayani Korogwe.
Akizungumza kwenye uzinduzi wa mradi huo, Mjumbe wa Kamati ya Kitaifa ya Hifadhi Hai Tanzania, Bw. Joseph Kibula alisema kuwa mradi huo ambao unatekelezwa katika maeneo ya Usambara Mashariki hapa nchini utawezesha wananchi wanaoishi kwenye vijiji vinavyozunguka hifadhi kutunza mazingira lakini kujiendeleza kiuchumi.
Kibula alisema nia kubwa ya mradi ni kukuza uchumi wa wananchi kwa kupitia njia zilizoboreshwa ambazo haziathiri rasilimali za misitu sambamba na kuanzisha biashara za kijani kwa ajili maendeleo endelevu ya wakazi wa maeneo hayo.
“Matarajio ni kuzijengea uwezo jamii za vijiji zenye bidhii ya kuhifadhi bioanuwai na kupunguza athari dhidi ya rasilimali za misitu …ili ziweze kutafuta riziki kwa maendeleo endelevu”,alisema Kibula.
Kwa upande wake, Afisa Mradi Kitengo cha Sayansi kutoka UNESCO na mwakilishi wa KOICA, Myoung Su Ko, alisema wanatarajia elimu hiyo ilete mabadiliko chanya kwa wananchi kaika kupunguza umaskini na kufanya biashara za kijani kwa maendeleo endelevu ya jamii wa Hifadhi Hai ya Usambara Mashariki.
Ko alisema kuwa kutokana na ushahidi wa huduma zitokanazo na bioanuwai,biashara ya kijani ni zana itakayowezesha kuhifadhi na kuleta maendeleo endelevu kupitia mgawanyo wa maslahi unaolingana.
DSC_0038
Afisa Mradi wa uchumi wa kijani ndani ya hifadhi hai (GEBR) Kitengo cha Sayansi kutoka UNESCO na mwakilishi wa KOICA, Myoung Su Ko akijumuika na baadhi ya wanakijiji wa Mnyuzi kucheza ngoma ya asili aina ya Mdumange kabla ya kufungua mafunzo hayo.
“Mradi huu unatoa fursa kwa jamii zilizopo na zilizopakana na hifadhi hai nchini Tanzania katika njia ya mazingira rafiki na uchumi wenye neema hususan Hifadhi Hai ya Usambara Mashariki…tunaamini kwa kupitia mradi huu na elimu hii mtaweza kujipatia utajiri mkubwa kwa kupitia shughuli za kiuchumi mtakazozifanya”,alisisitiza Mwakilishi huyo wa Unesco na Koica.
Nao baadhi ya wananchi waliopewa elimu hiyo walishukuru na kusema kuwa itawasaidia kupata mbinu za kufanya shughuli za kiuchumi kwa kutumia rasilimali zinazowazunguka.
“Katika utunzaji na uhifadhi wa mazingira tunafanya shughuli mbalimbali ikiwemo ufugaji wa nyuki,vipepeo na hata shughuli za mikono kwa akina mama hivyo elimu hii ya ujasiriamali itatuwezesha sana kujiinua kiuchumi na kuondokana na umaskini”,alisema Ayubu Rashid mkazi wa Kijiji cha Mnyuzi.
DSC_0046
Mkurugenzi Msaidizi wa Mambo ya Kale Taifa, Bw. John Kimaro ( wa pili kushoto) akifurahi jambo na Afisa Mradi wa uchumi wa kijani ndani ya hifadhi hai (GEBR) Kitengo cha Sayansi kutoka UNESCO na mwakilishi wa KOICA, Myoung Su Ko (kushoto) wakati wa burudani huku mgeni rasmi Mjumbe wa Kamati ya Kitaifa ya Hifadhi Hai Tanzania,Bw. Joseph Kigula (wa tatu kushoto) akingalia taswira mbalimbali alizochukua kupitia "Tablet" yake.
Kwa mujibu wa UNESCO asilimia 38 ya ardhi ya tanzania imekaliwa na misitu ambayo ni muhimu kayika maisha ya wanadamu na viumbe hai.
Hata hivyo inaaminika kwamba asilimia 75 ya watanzania wanaishi vijijini wakitegemea zaidi maliasili na kilimo.
Wamesema utegemezi huo umekuwa kikwazo kikubwa katika hifadi ya misitu ambayo imekuwa ikivamiwa kwa ajili ya mahitaji ya nishati na mbao.
Mradi wa GEBR unagusa wilaya ya Muheza, Mkinga, na Korogwe .
DSC_0073
Mkuu wa msafara wa ugeni huo Mhifadhi Hifadhi ya Mazingira asili Amani, Bi. Mwanaidi Kijazi akitoa utambulisho wa meza kuu kwa washiriki wa mafunzo hayo kutoka vijiji 19 (hawapo pichani) watakaonufaika na mradi huo.
DSC_0111
Mgeni rasmi Mjumbe wa Kamati ya Kitaifa ya Hifadhi Hai Tanzania, Bw. Joseph Kigula, akizungumza wakati akizindua rasmi mafunzo kwa washiriki kutoka vijiji 19 vinavyozunguka Hifadhi Hai ya usambara mashariki ikiwa ni utekelezaji wa mradi wa uchumi wa kijani ndani ya hifadhi hai(GEBR) unaoratibiwa na UNESCO kwa ufadhili wa KOICA. Kulia ni Mwenyekiti wa Kata ya Mnyuzi, Bw. Juma Mkunguti, Kutoka Kushoto ni Afisa Mradi wa Kitengo cha Sayansi kutoka UNESCO na mwakilishi wa KOICA, Myoung Su Ko, Mhifadhi Hifadhi ya Mazingira asili Amani, Bi. Mwanaidi Kijazi na Mkurugenzi Msaidizi wa Mambo ya Kale Taifa, Bw. John Kimaro.
DSC_0078
Afisa Mradi wa uchumi wa kijani ndani ya hifadhi hai (GEBR) Kitengo cha Sayansi kutoka UNESCO na mwakilishi wa KOICA, Myoung Su Ko (wa pili kushoto) akizungumza na washiriki na kuelezea lengo la mradi huo ambapo amesema unalenga kuwakomboa kiuchumi na kupunguza umaskini kwenye jamii zao. Wa tatu kushoto ni Mkuu wa msafara wa ugeni huo Mhifadhi Hifadhi ya Mazingira asili Amani, Bi. Mwanaidi Kijazi akitafsiri kwa washiriki.
DSC_0213
Mkufunzi wa Ujasiriamali/Biashara wa Program ya anzisha na imarisha biashara yako (SIYB) iliyochini ya Shirika la Kazi Duniani (ILO), Bw. Mussa Mashishanga akitoa mada ya namna ya kutafuta masoko kwenye mafunzo ya kuzijengea uwezo jamii za vijiji zenye bidii ya kuhifadhi bioanuwai na kupunguza athari dhidi ya rasilimali za misitu ili ziweze kutafuta riziki kwa maendeleo endelevu yanayofanyika kwenye Hoteli ya BS Palace kata Mnyuzi wilayani Korogwe.
DSC_0149
Pichani juu na chini ni Sehemu ya washiriki kutoka vijiji 19 vinavyozunguka Hifadhi Hai ya Usambara mashariki ikiwa ni utekelezaji wa mradi wa uchumi wa kijani ndani ya hifadhi hai(GEBR) wakifuatilia kwa umakini mafunzo hayo.
DSC_0128
DSC_0159
Mshauri na Mkufunzi wa Ujasiriamali/Biashara wa Program ya anzisha na imarisha biashara yako (SIYB) iliyochini ya Shirika la Kazi Duniani (ILO), Bw. Lawrence Ambokile akifafanua jambo kwa washiriki wakati wa mafunzo hayo.
DSC_0115
Mgeni rasmi Mjumbe wa Kamati ya Kitaifa ya Hifadhi Hai Tanzania Joseph Kigula (walioketi wa pili kulia) akiwa kwenye picha ya pamoja na wakufunzi pamoja na washiriki wa mafunzo hayo.
DSC_0114

0 comments