Thursday, 17 July 2014

Mshukiwa wa ugaidi mkenya akamatwa TZ

Mmoja wa watuhumiwa wa matukio ya ugaidi nchini Kenya,Jihad Gaibon Swaleh, amefikishwa mahakamani nchini Tanzania. 

Mshukiwa huyo amesomewa mashtaka ya kufadhili vitendo vya kigaidi nchini Kenya.
Pamoja naye watuhumiwa wengine 16 ambao wanadaiwa kuendesha vitendo vya kigaidi nchini Tanzania pia wamefikishwa mahakamani hii leo wakikabiliwa na tuhuma za kula njama ya kutenda makosa ya kigaidi nchini Tanzania.

Washtakiwa wote 17 wamerejeshwa rumande baada ya kusomewa mashtaka ya vitendo vya kigadi nchini Tanzania pamoja na nchi jirani ya Kenya.

Upande wa mashtaka ukiongozwa na mwendesha mashtaka ambaye ni wakili wa serikali mwandamizi Prosper Mwangamila ulidai mbele ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, kuwa kwa kutumia mtandao wa facebook aliweza kushawishi watu wengine kuwasiliana kwa lengo la kutafuta vifaa vya kulipua mabomu nchini Kenya na kusababisha majerahi, hofu na Vifo.

Jihand Gaibon Swaleh ambaye amesomewa mashtaka mawili hakuruhusiwa kukiri wala kukana mashitaka yanayomkabili kutokana na kwamba mashitaka hayo yanaangukia katika makosa ya ugaidi ambayo kwa mujibu wa sheria nchini Tanzania mahakama ya Hakimu Mkazi haina mamlaka ya kuendesha kesi za namna hiyo.

Katika kesi ya awali kutajwa mahakamani hapo washtakiwa wengine 16 walisomewa mashtaka mawili ikiwemo kula njama kutenda kosa pamoja na kushawishi wenzao kushiriki katika vitendo vya kigaidi katika sehemu mbali mbali nchini Tanzania. 

Ni makosa ambayo wanadaiwa kutenda kati ya Januari mwaka 2013 na Juni 2014 katika maeneo tofauti Tanzania.

Katika kesi zote mbili dhidi ya washtakiwa hao Upande wa mashtaka uliiambia mahakama iliyokuwa chini ya hakimu mfawidhi wa mahakama hiyo bi Hellen Riwa kuwa upelelezi bado unaendelea na hivyo kuiomba mahakama kuahirisha kesi hizo hadi mwishoni mwa mwezi huu wa Julai.

Awali mapema asubuhi msemaji wa jeshi la polisi nchini Tanzania Bi Advera John Bulimba aliwealeza waandishi wa habari kuhusu tuhuma dhidi ya washtakiwa hao

Hii ni mara ya kwanza kwa kundi kubwa la watuhumiwa kufikishwa mahakamani kwa pamoja wakikabiliwa na tuhuma za makosa ya kigaidi huku mtandao wa kijamii wa facebook nao ukitajwa kuhusika katika kutawanya taarifa za kuwezesha kutenda makosa hayo.



CHANZO: BBC SWAHILI

0 comments