WANAMUZIKI maarufu wa muziki wa taarabu, Khadija Omari Kopa na Shakila Said wameshirikiana pamoja katika kutengeneza wimbo wa Siku ya Msanii ulioimbwa na wasanii mbalimbali wa Tanzania, ambao umekamilika na umeanza kupigwa katika vituo mbalimbali vya redio nchini.
Mratibu wa Siku ya Msanii, Justine Jones alisema jana Dar es Salaam kwamba wimbo huo umerekodiwa katika Studio za Shillo zilizopo Boko, Dar es Salaam.
“Wimbo huu umeandaliwa maalumu kwa ajili ya kuitambulisha Siku ya Msanii, tumewaita wasanii wakongwe na chipukizi kwa ajili ya kutengeneza wimbo huu lengo ni kujenga umoja katika yao,” alisema Jones.
Jones aliwataka wasanii ambao wameshiriki kwenye wimbo huo mbali na Shakila na Kopa ni Hassan Rehani Bitchuka, Mhina Panduka, Tinner Malego, Abdul Salvador ‘Father Kidevu’, Yohana Luhanzo, Richard Mangustino, Joshua Bass, Ahmed Ahmed, Kilimatinde Mussa na Irene Sanga.
Akizungumzia Siku ya Msanii, Kopa alisema itawasaidia wasanii katika kutatua matatizo yao, kwani kwa muda mrefu wamekuwa hawana jukwaa la kusemea.
“Tunaishukuru Serikali kwa kuweza kutambua mchango wetu na kuitambua siku yetu, wasanii bado tunapaswa kuwa chombo kingine ambacho kitasaidia katika kutatua matatizo yetu,” alisema Kopa.
Siku ya Msanii Tanzania inaandaliwa na Kampuni ya Haak Neel Production kwa kushirikiana na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) na kudhaminiwa na New Habari (2006) Ltd, Channel Ten, Magic FM, Michuzi Media, PSPF, Proin Tanzania, Azam Media, CXC, Clouds FM, EFM na Ledger Plazza.
CHANZO: HABARI LEO
0 comments